Afisa Mzayuni apandishwa cheo kwa kufanya jinai kubwa Ghaza
Nduli mmoja wa utawala wa Kizayuni amepandishwa cheo kwa kufanya jinai kubwa zaidi dhidi ya watu wasio na hatia wa Ukanda wa Ghaza.
Shirika la Habari la Mehr limenukuu taarifa ya gazeti la Kizayuni la Haaretz ikisema kuwa, jeshi la Israel limempandisha cheo afisa wake huyo kutokana na kufanya jinai na uhalifu mkubwa zaidi dhidi ya raia katika Ukanda wa Ghaza.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, askari wengine wa Israel walitoa ushahidi kuwa afisa huyo wa Kizayuni ndiye aliyetoa amri ya kufyatuliwa risasi Wapalestina waliokuwa wameshika bendera nyeupe lakini pamoja na hayo, jeshi la utawala wa Kizayuni limempandisha cheo.
Wanajeshi waliokuwa chini ya uongozi wa afisa huyo Mzayuni katika Ukanda wa Ghaza walikiri kwamba alitoa amri ya kupigwa risasi na kuuliwa Wapalestina hao licha ya kwamba hawakuwa na hatari yoyote kwao.
Mwaka jana, mwandishi wa habari wa Israel, Chaim Har-Zahav, ambaye alihudumu katika kazi ya kuripoti vita vya Ghaza kwa muda wa siku 86 alieleza kwa kina kile alichoshuhudia wakati huo.
"Maisha ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza yanategemea kwanza kabisa kiwango cha maamuzi binafsi ya makamanda katika Ukanda huo," aliandika Har-Zahav na kuongeza kuwa, afisa mkuu yeyote anayeamuru kuuawa Wapalestina kwa sababu tu ya utambulisho wao, huwa hapewi adhabu yoyote ya kinidhamu.
"Maisha ya binadamu katika Ukanda wa Ghaza hayana thamani yoyote. Maisha ya maelfu ya mbwa wanaozurura ovyo kwenye eneo hilo kutafuta chakula yana thamani zaidi. Wakati kuna amri ya wazi inayokataza kuwapiga risasi mbwa isipokuwa askari akiwa yuko hatarini tena wakati meno ya mbwa yamemkaba, wanajeshi wa Israel wameruhusiwa kumpiga risasi Mpalestina yeyote na bila ya woga wala kizuizi chochote," aliandika.
Leo hii na licha ya kuweko ushahidi wa kutosha wa kutenda jinai kubwa afisa huyo wa jeshi la Israel, lakini amepandishwa cheo na kupongezwa kwa jinai zake kubwa zaidi huko Ghaza.