Hamas: Israel imefanya uharamia kwa kushambulia meli ya misaada
Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina (Hamas) imelaani shambulio la utawala wa Kizayuni dhidi ya meli iliyobeba misaada ya kibinadamu kuelekea Gaza na kusema kuwa, kitendo hicho ni uharamia wa baharini na jinai dhidi ya binadamu.
Hamas imetoa wito wa kuachiliwa huru mara moja wanaharakati wote waliotekwa nyara na kuuwajibisha utawala wa Kizayuni kwa ajili ya usalama wao.
Harakati hiyo ya kupigania ukombozi wa Palestina imeutaka Umoja wa Mataifa na mashirika ya kimataifa kulaani uhalifu huo na kuchukua hatua kukomesha mzingiro wa Gaza.
Imesisitiza kuwa, kukamatwa na kuzuiwa kwa utoaji wa misaada ya kiishara kwa watu wanaokabiliwa na mauaji ya kimbari Gaza kunajumuisha "ugaidi wa serikali uliopangwa," ukiukwaji wa wazi wa sheria za kimataifa, na shambulio la kujitolea la kiraia linaloendeshwa na nia ya kibinadamu.
Hatua hiyo imeibua hisia nyingi za kimataifa na inachukuliwa kuwa ni ukiukaji wa wazi wa sheria za baharini na haki za binadamu. Kuendelea kuzingirwa kwa Gaza na kunyakuliwa kwa misaada ya kibinadamu kumezusha wasiwasi mkubwa kuhusu hali mbaya ya kibinadamu katika eneo hilo.
Wanajeshi wa utawala katili wa Israel wamewateka nyara wanaharakati waliokuwa ndani ya meli hiyo ya misaada ya kibinadamu Madleen iliyokuwa ikielekea Gaza, Jumapili usiku.

Huku hayo yakiarifiwa, mpango mkubwa unaohusisha wafanyakazi wa kujitolea kutoka Afrika Kaskazini unajiandaa kuelekea Palestina kupitia Misri, kwa lengo la kuvunja mzingiro wa Israel dhidi ya Gaza na kutoa msaada muhimu wa kibinadamu kwa watu wa Gaza.
Maelfu ya watu waliojitolea kutoka Morocco, Algeria, Tunisia, Libya na Misri wanajipanga kukabiliana na mzingiro wa Israel, ambao umezuia kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa bidhaa muhimu kwa watu wa Gaza.