Ansarullah kupanua wigo wa operesheni zake dhidi ya Israel
Harakati ya Ansarullah ya Yemen imetangaza kuwa itapanua wigo wa operesheni zake dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel.
Saa chache baada ya utawala haramu wa Israel kushambulia bandari ya Hudeidah iliyoko magharibi mwa Yemen, Harakati ya Ansarullah ya Yemen imetangaza kuwa itapanua wigo wa operesheni zake dhidi ya utawala huo ghasibu.
Nasreddin Amer, Naibu Mkuu wa Baraza la Habari la Harakati ya Ansarullah ametuma ujumbe kwenye mtandao wa kijamii wa X (zamani Twitter) na kuandika: "Uchokozi wa utawala wa Kizayuni kwenye bandari ya Hudeidah haujaleta athari kubwa katika operesheni ya kuunga mkono Ghaza, na haujaathiri ari ya watu wetu, wanaounga mkono Gaza kwa kuadamana kwa mamilioni kila wiki."
Amer amesisitiza kwamba, shambulio hilo la Wazayuni halijazuia wala kuathiri maandalizi ya kuimarisha na kupanua operesheni dhidi ya maeneo ya ndani kabisa ya Palestina yanayokaliwa kwa mabavu.
"Vizuizi vya majini vya utawala wa Kizayuni na Yemen, ambavyo vimesababisha kufungwa kabisa kwa bandari ya Umm al-Rishrash (Eilat), havitaondolewa, wala marufuku ya safari za ndege katika Uwanja wa Ndege wa Lod (Ben Gurion), ambayo imesababisha mashirika mengi ya ndege duniani kusitisha safari zao kuelekea katika viwanja vya ndege vya adui, haitaondolewa," ameongeza.
Haya yanajiri katika hali ambayo, Jeshi la Yemen limeyashambulia maeneo muhimu ya utawala wa Kizayuni na kuufanya mfumo wa kujilinda na mashambulizi ya makombora wa Israel uchanganyikiwe na kulazimika kufyatua takriban makombora 10 kukabiliana na kombora moja la Yemen.