Shakhsia wa kidini Bahrain wazidi kuswekwa korokoroni
Polisi ya utawala wa Aal-Khalifa nchini Bahrain imewatia mbaroni wanazuoni wanne mashuhuri wa Kiislamu, katika kile kinachoonekana ni muendelezo wa dhulma na ukandamizaji dhidi ya Waislamu wa madhehebu ya Shia nchini humo.
Miongoni mwa waliokamatwa katika wimbi jipya la kamatakamata ya polisi ya Bahrain ni Sheikh Issa Momen, Imam wa Swala ya Ijumaa katika Msikiti wa Khayf katika kitongoji cha Dair, mashariki mwa mji mkuu Manama.
Shakhsia wengine wa Kiislamu waliokamatwa na polisi ya Bahrain ni Sheikh Ali al-Hamli, Sayyid Mohsen Qarifi na Sheikh Fazil Zaki waliokamatwa mashariki mwa mji wa Manama.
Agosti Pili, Maulamaa wa Bahrain akiwemo Sheikh Issa Qasim na Sayyid Abdullah al-Ghuraibi walitoa taarifa na kuwataka viongozi wa utawala wa Aal-Khalifa wamwachilie huru Sayyid Majid al-Mash'al, Mkuu wa Baraza la Maulamaa wa Kiislamu la nchi hiyo pamoja na shakhsia wengine wa kidini na wasio wa kidini walioko kwenye jela za utawala huo. Vikosi vya usalama vya utawala wa Aal Khalifa, asubuhi ya tarehe 30 Julai viliivamia nyumba ya Sheikh Majid al-Mash'al na kumtia nguvuni alimu huyo wa Kishia bila ya kumueleza sababu wala tuhuma zinazomkabili.
Tangu mwezi Februari mwaka 2011, Bahrain imekuwa uwanja wa maandamano ya amani ya kupinga utawala wa kifalme wa ukoo wa Aal Khalifa. Wananchi wa Bahrain wanataka uhuru, kutekelezwa uadilifu, kuondolewa ubaguzi na kuweko madarakani utawala uliochaguliwa na wananchi wenyewe.