IPOA yafichua: Polisi wa Kenya waliua watu 65 katika maandamano Juni, Julai
Ripoti mpya ya Mamlaka Huru ya Kuchunguza Utendakazi wa Polisi (IPOA) imefichua kwamba watu 65 walipoteza maisha, 41 kati yao kwa kupigwa risasi na maafisa wa polisi, huku raia 342 wakijeruhiwa vibaya wakati wa maandamano ya Juni 25 na Julai 7 mwaka huu dhidi ya serikali ya Rais William Ruto wa Kenya.
Haya ni miongoni mwa matokeo yaliyotajwa katika ripoti ya Julai 2025 ya IPOA iliyopewa jina “Ripoti ya kufuatilia Majibu ya Polisi kwa Maandamano ya Umma kati ya Juni na Julai 2025”.
Ripoti hiyo imesema, kwa jumla, watu zaidi ya 90 walipigwa risasi baadhi kwenye kifua, tumbo, hata kichwani. Licha ya idadi kubwa ya vifo, IPOA imelaumu Huduma ya Kitaifa ya Polisi kwa kuripoti vifo vitano pekee kati ya 65.
IPOA imesema kutotoa ripoti kamili kwa makusudi ni ukiukaji wa wajibu wa uwajibikaji, na kunadhihirisha hulka ya taasisi hiyo ya kuficha ukweli.
Ili kuthibitisha chanzo cha vifo hivyo, IPOA ililazimika kushiriki upasuaji wa miili 61 ikijitegemea.

Mamlaka hiyo imeonya kuwa kuficha taarifa kunahujumu haki na kunaleta dhana kwamba polisi wa Kenya wako juu ya sheria.
Ripoti hiyo haiishii kuhesabu walioumia pekee, bali inafichua mapungufu ya kimuundo ya jinsi serikali ya Kenya ilivyoshughulikia maandamano, ikianika mfumo wa polisi ulio katika hali ya mgogoro mkubwa.
“Majibu ya polisi yalikuwa ya kikatili, mara nyingi ya kifo,” imesema ripoti hiyo na kuongeza kuwa: Hata baada ya amri ya mahakama kutaka polisi wavalie sare rasmi na vitambulisho vinavyoonekana, maafisa wengi walionekana wakifanya kazi bila nambari za kuwatambua, wakiwa wameficha uso.
Hali hiyo ilikiuka moja kwa moja Sheria ya Polisi (CAP 84), na kuwaacha waathiriwa wa ukatili wa polisi bila njia ya kuwatambua au kuwafungulia mashtaka waliowadhuru.