Yemen yazamisha meli nyingine ikielekea Israel katika Bahari Nyekundu
Yemen imeshambulia meli nyingine iliyokuwa inaelekea Israel, ili kuwaunga mkono Wapalestina wanaokabiliwa na mauaji ya halaiki katika Ukanda wa Gaza.
Katika taarifa yake jana Jumatano, Jeshi la Yemen limetangaza kuwa kikosi chake cha majini "kililenga meli ya 'ETERNITY C', iliyokuwa ikielekea bandari ya Umm al-Rashrash (Eilat) katika ardhi ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu", baada ya wafanyakazi wake kupuuza maonyo na wito uliotolewa na vikosi hivyo vya baharini.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, operesheni hiyo ya kijeshi ilifanywa kwa "chombo kisicho na rubani na makombora sita ya baharini na ya balestiki."
Taarifa hiyo imesisitiza kuwa, meli hiyo "ilizama kikamilifu", na kwamba operesheni hiyo "imenakiliwa kwenye mikanda ya sauti na video. " Wafanyakazi hao, hata hivyo, "waliokolewa" na "kusafirishwa hadi mahali salama" na vikosi vya Yemen, imesisitiza taarifa hiyo.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa, marufuku iliyowekwa kwa meli zinazofungamana na Israel katika Bahari Nyekundu na Arabia bado ipo, ikionya makampuni dhidi ya kujihusisha na miamala au shughuli zinazohusisha bandari za Israel.
Jeshi la Yemen limesisitiza kuwa, kuunga mkono operesheni za Gaza na Palestina zitaendelea kwa kasi kubwa, na kwamba Wayemen watailinda nchi yao, na taifa lao kwa nguvu zote.