Oxfam yaonya kuhusu janga la binadamu Gaza
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i128714-oxfam_yaonya_kuhusu_janga_la_binadamu_gaza
Shirika la kimataifa la Oxfam limeonya kuwa, maafa ya binadamu katika Ukanda wa Gaza yamefikia kiwango kisicho na kifani na njaa imeenea katika eneo zima.
(last modified 2025-07-24T23:02:31+00:00 )
Jul 24, 2025 23:02 UTC
  • Oxfam yaonya kuhusu janga la binadamu Gaza

Shirika la kimataifa la Oxfam limeonya kuwa, maafa ya binadamu katika Ukanda wa Gaza yamefikia kiwango kisicho na kifani na njaa imeenea katika eneo zima.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari Oxfam imesisitiza kuwa njaa imegharimu maisha ya raia wengi na kwamba maafa ya binadamu yanatokea katika Ukanda wa Gaza huko Palestina.

Taarifa hiyo imesema kuwa, watu wa Gaza wanakabiliwa na majanga makubwa ikiwa ni pamoja na utapiamlo na uchafuzi wa maji, masuala ambayo yamezidisha mateso yao katika hali mbaya ya sasa na isiyo na kifani.

Tamko la Oxfam linakuja wakati ambao vivuko vya Gaza vimefungwa kabisa kwa zaidi ya siku 140, hatua ambayo imechukuliwa na utawala unaoikalia kwa mabavu Palestina licha ya kuweko makubaliano ya hapo awali ya kusitisha mapigano na kubadilishana mateka.

Wizara ya Afya ya Gaza imetangaza kuwa katika muda wa saa 24 pekee zilizopita, watu wengine 10 wameaga dunia kutokana na njaa na utapiamlo. Kwa muktadha huo, idadi ya wahanga wa njaa imefikia 111, takwimu ambazo wataalamu wa mambo wanasema zinaweza kuongezeka katika siku zijazo. Takwimu hizi za kutisha zinathibitisha kuwa mbaya hali ya kibinadamu na shida ya chakula katika eneo hilo, ambayo imechangiwa pakubwa na mzingiro na vita vya muda mrefu vinavyoendeshwa na utawala wa kizayuni wa Israel unaoungwa mkono na Marekani na washirika wake.