UNICEF: Watoto wanafariki Ghaza kwa kasi ambayo 'haijawahi kushuhudiwa'
Aug 02, 2025 13:16 UTC
Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) limeitaka jamii ya kimataifa ichukue hatua za haraka ili kuzuia vifo vingi vya watoto katika Ukanda wa Ghaza, ambako hali inaendelea kuwa mbaya wakati huu wa vita vinavyoendelezwa na utawala wa kizayuni wa Israel dhidi ya eneo hilo uliloliwekea mzingiro.
Ted Chaiban, Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF amesema: "leo ninataka kuweka mkazo juu ya Ghaza, kwa sababu ni huko Ghaza ambako mateso ni makali zaidi na watoto huko wanakufa kwa kasi ambayo haijawahi kushuhudiwa".
Chaiban ambaye alikuwa anaelezea kuhusu ziara yake fupi aliyofanya hivi majuzi katika Mashariki ya Kati ameendelea kueleza: "tuko katika njia panda, na chaguo litakalofanywa sasa hivi ndilo litakaloamua iwapo makumi ya maelfu ya watoto wataishi au watakufa".
Katika safari yake hiyo iliyohusisha 'Israel' na maeneo yote mawili ya Palestina yanayokaliwa kwa mabavu ya Ghaza na Ukingo wa Magharibi, Chaiban amesema ziara yake hiyo ilikuwa ya nne huko Ghaza tangu vita vya kinyama vya utawala wa kizayuni dhidi ya eneo hilo vilipoanza Oktoba 7, 2023.
"Unaona picha kwenye habari, na unajua nini kimetokea, lakini bado inashangaza ukiwa huko; alama za mateso makubwa na njaa zinaonekana kwenye nyuso za familia na watoto," ameeleza afisa huyo mwandamizi wa UNICEF.
Amekumbusha kuwa zaidi ya watoto 18,000 wameshauawa huko Ghaza tangu vita vilipoanza.
Chaiban amesema: "Ghaza sasa inakabiliwa na hatari kubwa ya njaa. ... Mtu mmoja kati ya watatu huko Ghaza anaishi siku nyingi bila chakula, na kiashiria cha utapiamlo kimevuka kiwango cha njaa, huku utapiamlo wa hali ya juu duniani sasa ukiwa zaidi ya asilimia 16.5. Leo, zaidi ya watoto wadogo 320,000 wako katika hatari ya kupata utapiamlo mkali".
Amesisitiza kuwa, kinachofanyika katika mazingira halisi ni hali ya "ukatili" na kuongeza kuwa kile ambacho watoto wanahitaji katika jamii zote ni usitishaji mapigano wa kudumu na kusonga mbele kupitia utatuzi wa kisiasa.../
Tags