Indonesia: Mataifa ya dunia yanapaswa kuitambua rasmi Palestina
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i129388
Indonesia imelaani mpango wa utawala wa Israel wa kuikalia kwa mabavu Gaza na kuzitaka nchi zote kulitambua taifa huru la Palestina.
(last modified 2025-08-11T05:05:57+00:00 )
Aug 11, 2025 02:41 UTC
  • Indonesia: Mataifa ya dunia yanapaswa kuitambua rasmi Palestina

Indonesia imelaani mpango wa utawala wa Israel wa kuikalia kwa mabavu Gaza na kuzitaka nchi zote kulitambua taifa huru la Palestina.

Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Indonesia imeandika kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa X: "Mpango wa Israel wa kuikalia kwa mabavu Gaza unakiuka kwa kiasi kikubwa sheria za kimataifa na Mkataba wa Umoja wa Mataifa, na unazidisha mzozo wa kibinadamu katika ukanda huo na kufifiza matarajio ya amani katika eneo hilo."

Taarifa ya wizara hiyo imeongeza kuwa: "Kama ambavyo Mahakama ya Kimataifa ya Uadilifu imetangaza wazi kuwa, uvamizi wa Israel katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu ni kinyume cha sheria na Israel haina mamlaka ya kutawala katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu. Kwa hiyo, hakuna hatua yoyote ya Israel inayoweza kubadilisha hadhi ya kisheria ya ardhi za Palestina."

Kadhalika Indonesia imetoa wito kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na jamii ya kimataifa kuchukua "hatua madhubuti" kukomesha vitendo haramu vya utawala vamizi wa wa Israel.

Sehemu nyingine ya taarifa ya Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Indonesia imesisitiza kuwa, mataifa ya dunia yanapaswa kuitambua rasmi Palestina na kuchukua hatua za kukabiliana na hatua za utawala ghasibu wa Israel za kukiuka haki za binadamu na kufanya jinai dhidi ya binadamu katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu.

Licha ya miito ya kila leo ya kukomeshwa jinai za Israel katika Ukanda wa Gaza, utawala ghasibu wa Israel ukipata himaya na uungaji mkono wa Marekani umeendelea kufanya mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina huku Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa likishindwa kuchukua hatua ya maana ya kukomesha mauaji hayo.