Larijani awasili Beirut/ Iran daima itakuwa upande wa taifa azizi la Lebanon
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i129478-larijani_awasili_beirut_iran_daima_itakuwa_upande_wa_taifa_azizi_la_lebanon
Ali Larijani, Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran alisema jana jioni mara tu baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa Beirut, mji mkuu wa Lebanon, kuwa Iran na Lebanon zina ustaarabu wa kina na kuwa zimekuwa na uhusiano wa karibu tangu karne nyingi zilizopita.
(last modified 2025-08-13T03:47:25+00:00 )
Aug 13, 2025 03:47 UTC
  • Larijani awasili Beirut/ Iran daima itakuwa upande wa taifa azizi la Lebanon

Ali Larijani, Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran alisema jana jioni mara tu baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa Beirut, mji mkuu wa Lebanon, kuwa Iran na Lebanon zina ustaarabu wa kina na kuwa zimekuwa na uhusiano wa karibu tangu karne nyingi zilizopita.

Amesema safari za aina hii zinaweza kuandaa uwanja wa kufanyika uratibu zaidi kati ya Tehran na Beirut katika nyanja za ulinzi, mabadilishano ya habari na masuala ya kisiasa.

Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran amepangiwa kukutana na kuzungumza na viongozi wa ngazi za juu wa Lebanon akiwemo Spika wa Bunge na Rais wa nchi hiyo.

Ameongeza kuwa uhusiano wa kiutamaduni kati ya Iran na Lebanon umeimarisha uhusiano kati ya mataifa haya mawili na kwamba Iran daima itakuwa pamoja na taifa la Lebanon.

Nafasi ya Iran katika kuunga mkono makundi ya muqawama na kuwezesha maingiliano na taasisi rasmi za Lebanon daima limekuwa likitazamwa kwa jicho la wasiwasi na wadau wengine wa kieneo na kimataifa.

Masuala ya kikanda na ushirikiano wa nchi mbili ni suala litakalopewa kipaumbele muhimu katika ajenda ya mazungumzo hayo.

Afisa huyo wa ngazi ya juu wa usalama wa Iran amesafiri Lebanon katika kile kimetajwa kuwa safari muhimu ya kujadili wasiwasi kuhusu usalama wa Lebanon huku kukiwa na mashinikizo ya Marekani ya kutaka Hizbullah ya Lebanon ipokonywe silaha kwa maslahi ya utawala ghasibu wa Israel, hatua inayopingwa na raia wengi wa nchi hiyo.

Ziara hiyo inakuja takriban wiki moja baada ya baraza la mawaziri la Lebanon kuidhinisha pendekezo la Marekani la kupokonywa silaha Hizbullah ifikapo mwishoni mwa mwaka huu.

Hizbullah imelaani uamuzi huo wa serikali na kusema ni "dhambi kubwa," ikionya kwamba uamuzi huo unadhamini kikamilifu maslahi ya utawala wa Israel.

Uchunguzi wa maoni wa hivi karibuni, hata hivyo, umegundua kuwa wengi wa Walebanon wanapuuzilia mbali suala hilo la upokonyaji silaha na kuamini kuwa jeshi la nchi hiyo pekee halina uwezo wa kukabiliana na vitendo vya uchokozi vya utawala wa Israel.

Harakati hiyo muqawama ilifanikiwa kupigana vita viwili vya pande zote na Israel katika miaka ya 2000 na 2006.

Mnamo mwaka 2023, ilianzisha mashambulizi ya mshikamano na Wapalestina katika Ukanda wa Gaza dhidi ya utawala wa Israel, ambao wangali wanakabiliwa na mauaji ya umati na jinai za kutisha kutoka kwa utawala huo katili.