Hizbullah na Amal zatoa wito wa maandamano makubwa ya kupinga kupokonywa silaha makundi ya muqawama
Harakati za muqawama za Hizbullah na Amal za Lebanon zimetoa wito kwa wafuasi wao kujitokeza kwa wingi katika mitaa ya Beirut mji mkuu wa nchi hiyo ili kupinga maamuzi ya hivi karibuni ya baraza la mawaziri ya kuyapokonya silaha makundi ya Muqawama.
Ofisi mbili za kazi za makundi hayo ya muqawama zimewatolea wito wafanyakazi, makundi, na matabaka mbalimbali ya wananchi wa Lebanon kukutana kesho Jumatano saa kumi na moja na nusu alasiri katika maidani ya Riad al Solh huko Beirut kupinga maamuzi mawili ya karibuni ya serikali.
Harakati ya Hizbullah na ile ya Amal zimesema katika taarifa yao ya pamoja kuwa maandamano hayo yana maana ya kupinga maamuzi ya baraza la mawaziri la Lebanon yaliyochukuliwa mapema mwezi huu.
Makundi hayo ya muqawama yameyataja maamuzi hayo kuwa ni kinyume na maslahi ya taifa ya Lebanon na msingi wa kuishi pamoja.
Taarifa ya Hizbullah na Amal imebainisha kuwa: Maandamano waliyoitisha kesho huko Beirut yatafanyika kwa madhumuni ya kuhami mamlaka ya kujitawala, kutetea uhalali wa mapambano ya silaha dhidi ya Israel na kukataa mashinikizo kutoka nje katika ardhi ya Lebanon.