UNRWA: Zaidi ya wakimbizi laki moja wa Gaza hawajapokea msaada wowote tangu miezi 6 iliyopita
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i130676-unrwa_zaidi_ya_wakimbizi_laki_moja_wa_gaza_hawajapokea_msaada_wowote_tangu_miezi_6_iliyopita
Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) limetangaza kuwa, zaidi ya watu laki moja wanaendelea kutaabika na njaa katika maeneo ya kuwahifadhi wakimbizi ya shirika hilo huko Gaza, na hakuna msaada wa kibinadamu ambao umeruhusiwa kuingia katika eneo hilo kwa zaidi ya miezi 6 sasa.
(last modified 2025-09-11T11:04:17+00:00 )
Sep 11, 2025 11:04 UTC
  • UNRWA: Zaidi ya wakimbizi laki moja wa Gaza hawajapokea msaada wowote tangu miezi 6 iliyopita

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) limetangaza kuwa, zaidi ya watu laki moja wanaendelea kutaabika na njaa katika maeneo ya kuwahifadhi wakimbizi ya shirika hilo huko Gaza, na hakuna msaada wa kibinadamu ambao umeruhusiwa kuingia katika eneo hilo kwa zaidi ya miezi 6 sasa.

Shirika la UNRWA linasisitiza kuwa bado lipo Gaza na kwamba timu za matibabu za shirika hilo zinaendelea kutoa ushauri wa masuala ya afya kwa raia katika ukanda huo. 

Shirika hilo la Umoja wa Mataifa limesema katika ujumbe wake uliotumwa katika mtandao wa kijamii wa "X" kwamba zaidi ya wakimbizi 100,000 bado wanaishi katika makazi ya shirika hilo huko Gaza. 

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, wakimbizi wa Gaza "wamechoka sana na wanateseka kwa njaa kali" na hakuna msaada wa kibinadamu ulioruhusiwa kuingia katika eneo hilo kwa zaidi ya miezi sita sasa. 

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) limesisitiza  kuhusu dhamira yake ya kuendelea kutoa huduma, licha ya changamoto za kibinadamu ambazo hazijawahi kushuhudiwa. Limesisitiza kuwa kuna udharura wa kusitishwa vita huko Gaza. 

Leo Alhamisi shirika la UNRWA limetuma ujumbe wake mwingine na kutangaza kuwa oparesheni ya kijeshi ya Israel katika mji wa Gaza imewakosesha watu makazi.  

Wakati huo huo UNRWA imetoa indhari katika ukurasa wake rasmi wa Facebook ikisema: "Watu hawana pa kwenda, hakuna mahali salama wala mtu aliye salama katika Ukanda wa Gaza."