Wimbi jipya barani Afrika la kuunga mkono Palestina na kulaani Israel
Wananchi na viongozi wa nchi za Kiafrika wamelaani jinai za Israel katika wimbi jipya la kuwaunga mkono Wapalestina.
Raia wa nchi kadhaa za Kiafrika walionyesha uungaji mkono mkubwa kwa Wapalestina huku wakilaani jinai kubwa za Israel dhidi ya wakaazi wa Ukanda wa Gaza katika vita vya Gaza. Sambamba na hayo, viongozi wa baadhi ya nchi za Kiafrika pia wamelaani jinai za Israel na kuunga mkono kadhia ya Palestina.
Katika muktadha huo, watu zaidi ya elfu tatu waliandamana siku ya Jumamosi katika mji wa Cape Town Afrika Kusini wakiitaka nchi hiyo kukata uhusiano wa kibiashara na kidiplomasia na Israel, ikiwa ni pamoja na kufunga ubalozi wake kufuatia vita na mauaji ya kimbari yanayotekelezwa na utawala huo katika Ukanda wa Gaza.
Maandamano ya Cape Town, Afrika Kusini yalizikutanisha pamoja taasisi kadhaa zinazoiunga mkono Palestina, vyama vya kisiasa na makundi ya Waislamu na Wakristo. Maandamano hayo yametajwa kuwa moja kati ya maandamano makubwa kuwahi kushuhudiwa nchini Afrika Kusini katika miezi ya karibuni.
Wakiwa wamebeba bendera za Palestina, washiriki wa maandamano hayo walipiga nara za kuunga mkono Gaza na kutaka kuchukuliwa hatua za kivitendo badala ya kuonyesha kuwaunga mkono tu watu wanaodhulumiwa wa Gaza. Mwishoni mwa maandamano hayo, waandamanaji waliwasilisha takwa lao kwa Bunge la Afrika Kusini.
Hii ni katika hali ambayo, Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini akizungumza katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York siku ya Jumatano alikosoa kitendo cha utawala wa Kizayuni kupuuza sheria za kimataifa na hukumu za Mahakama ya Kimataifa ya Jinai na kutaka kuchukuliwa hatua za kimataifa kukabiliana na mauaji ya kimbari ya Israel katika Ukanda wa Gaza.

Katika hatua nyingine, Wamorocco waliandamana huko Tangier na kuunga mkono msafara wa meli unaobeba misaada ya kibinadamu wa Sumud kwa ajili ya kuvunja mzingiro dhidi ya Ukanda wa Gaza.
Washiriki wa mkusanyiko huo wakiwa wamebeba mabango na maberamu walitoa mwito wa kukomeshwa mauaji ya halaiki na kuunga mkono msafara wa Sumud Flotilla. Mji wa Marrakesh (katikati ya Morocco) pia ulishuhudia mkusanyiko kama huo, ambao ulifanyika kwa mwaliko wa "Kambi ya Morocco ya Kuunga Mkono Palestina.
Uungaji mkono wa pande zote wa wananchi wa Morocco kwa Wapalestina umeilazimu serikali ya Rabat ambayo imeanzisha uhusiano wa kisiasa na utawala wa Kizayuni kuchukua msimamo kuhusu suala hili. Kuhusiana na suala hilo Aziz Akhannouch, Waziri Mkuu wa Morocco alitoa wito wa kusitishwa mara moja mapigano katika Ukanda wa Gaza na kuanza tena mazungumzo wakati alipotoa hotuba yake kwenye Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa,.
Amesisitiza kufunguliwa ukurasa mpya wa utatuzi wa kisiasa wa kadhia ya Palestina na ulazima wa kuandaa jedwali kwa ajili ya kutambua haki za kisheria za watu wa Palestina na kuanzishwa taifa huru la Palestina.
Huku akisisitiza kwamba jamii ya kimataifa lazima ifanye juhudi kubwa zaidi kuliondoa eneo hilo kutoka katika giza hilo totoro Akhannouch alitoa wito wa kuingizwa bila masharti kwa misaada ya kibinadamu katika Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi.
Mohamed Ali Al-Nafti, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Tunisia, katika hotuba yake katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa alikosoa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa kutokuwa na uwezo wa kuhitimisha vita vikali vya utawala wa Kizayuni dhidi ya watu wa Gaza na kuvitaja kuwa ni chanzo cha "ghadhabu na mkanganyiko kati ya mataifa."
Kadhalika Rais Taye Atske Selassie wa Ethiopia alisisitiza haki ya watu wa Palestina ya kujitawala wakati alipohutubia kikao cha 80 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

Kiujumla, mtazamo wa Waafrika, hususan katika nchi za Kiislamu za bara hilo, kuhusiana na Israel ni mchanganyiko wa mshikamano wa kihistoria na Palestina, uzoefu wa ukoloni, na athari za kijiografia za kisasa. Mtazamo huu unaweza kufupishwa katika nukta kadhaa kuu:
Mshikamano wa kihistoria na Palestina
- Nchi nyingi za Kiafrika, hasa zile ambazo zimepitia tajiriba ya ukoloni na mapambano ya kudai uhuru, zinajihesabu kuwa zina hatima ya pamoja na watu wa Palestina.
- Viongozi wa ukombozi wa Afrika kama vile Nelson Mandela wameunga mkono mara chungu nzima harakati za Palestina na kulinganisha uvamizi wa Israel na utawala wa makaburu wa ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini.
Misimamo ya nchi za Kiislamu za Kiafrika
- Nchi za Kiislamu kama vile Sudan, Mali, Mauritania na Algeria kawaida huwa na misimamo mikali zaidi dhidi ya Israel na hutetea haki za Wapalestina.
- Hata hivyo, baadhi ya nchi kama vile Morocco na Sudan, zimeanzisha uhusiano wa kawaida na Israel katika miaka ya hivi karibuni, chini ya mashinikizo ya kidiplomasia na kiuchumi, hatua ambayo imekabiliwa na maoni hasi ya umma katika nchi hizo.
Maoni ya umma na vyombo vya habari
- Katika jamii nyingi za Kiafrika, hususan kati ya Waislamu, Israel inatambuliwa kuwa nembo ya ukandamizaji na uvamizi.
- Vyombo vya habari vya ndani na mitandao ya kijamii katika nchi za Kiafrika mara nyingi huangazia habari kuhusu mashambulizi ya Israel dhidi ya Gaza na Yemen kwa sauti ya kukosoa, na huruma kwa wahanga wa Palestina ni jambo la kawaida.
Pengo kati ya misimamo rasmi ya serikali na ya wananchi
- Katika hali ambayo, baadhi ya serikali za Kiafrika zimepanua uhusiano wao na Israeli kwa sababu za kiuchumi au kisiasa, maoni ya umma katika nchi nyingi za bara hilo yanaendelea kukosoa Israel.
- Pengo hili limesababisha baadhi ya serikali kuchukua misimamo ya tahadhari zaidi katika majukwaa ya kimataifa ili kuepusha radiamali za ndani.