Lieberman: Israel si lolote si chochote bila ya msaada wa Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i133176-lieberman_israel_si_lolote_si_chochote_bila_ya_msaada_wa_marekani
Waziri wa zamani wa fedha wa utawala wa Kizayuni amekiri kwamba hivi sasa Israel inapitia kipindi kibaya mno cha kiuchumi na kusisitiza kwamba inabidi waishukuru Marekani kwa msaada wake kwani bila ya msaada huo, Israel si lolote si chochote, bali itaangamia.
(last modified 2025-11-14T23:04:53+00:00 )
Nov 14, 2025 23:04 UTC
  • Avigdor Lieberman (kulia) na Netanyahu


9
    Avigdor Lieberman (kulia) na Netanyahu 9

Waziri wa zamani wa fedha wa utawala wa Kizayuni amekiri kwamba hivi sasa Israel inapitia kipindi kibaya mno cha kiuchumi na kusisitiza kwamba inabidi waishukuru Marekani kwa msaada wake kwani bila ya msaada huo, Israel si lolote si chochote, bali itaangamia.

Avigdor Lieberman ambaye pia ni kiongozi wa chama cha Kizayuni cha Yisrael Beiteinu amesema hayo kwenye mahojiano na shirika la habari la Walla na kukosoa vikali sera za kiuchumi za serikali ya Netanyahu akikiri waziwazi kwamba hivi sasa Israel imetengwa katika jamii ya kimataifa hususan kwenye masuala ya kiuchumi.

Amesema: "Serikali iliyoko madarakani Israel inaunga mkono kukandamizwa wananchi kwa kodi na inapinga biashara - na hiyo ndiyo sifa yake kuu."

Amesema kwa kusisitiza kwamba: "Tumetengwa katika jumuiya ya kiuchumi ya kimataifa; wakati mfuko wa utajiri wa Norway unapoamua kuondoka Israel, ni onyo kubwa kwetu."

Amedai kwamba utawala wa Kizayuni una uwezo mkubwa lakini kwa sharti la kuwa na uongozi sahihi. Aidha amedai kwamba utawala huo unaweza kuizidi Uswisi kwa viwango vya maisha na nguvu ya kiuchumi katika kipindi cha miaka mitano hadi sita, ikiwa serikali ya Netanyahu itaangushwa."

Kwa upande wake, Moshe Feiglin, mkuu wa chama cha Zehut ambaye pia ni mkosoaji wa sera za Netanyahu amesema: "Netanyahu amesalimisha uhuru na kuigeuza Israel kuwa tegemezi. Tusingekuwa na nguvu zozote huko Ghaza na Lebanon bila ya msaada wa Marekani."

Kiongozi wa upinzani na waziri mkuu wa zamani wa Israel, Yair Lapid pia amemkosoa Netanyahu akiandika: Sisi si wa kuitegemea serikali ya Marekani. Waziri mkuu hapaswi kukimbilia kwa Trump kila wakati kuomba msaada."

Anthony Lowenstein, mwandishi wa habari na veterani wa vita wa Israel alikiri waziwazi katika mahojiano na Al Jazeera ya Oktoba 8, 2024, akisema: "Ukweli wa wazi ni kwamba Israel haiwezi kupigana vita vyovyote bila ya Marekani."