Iran yalaani jinai zinazotendwa nchini Sudan
-
Ali Bahraini, balozi na mwakilishi wa kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Geneva
Iran imepaza sauti kulaani “jinai na ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu” unaoendelea nchini Sudan, ikisisitiza kuwa hali ya kibinadamu katika mji wa Al-Fasher na maeneo jirani imefikia kiwango cha hatari kinachohitaji msaada wa haraka wa jumuiya ya kimataifa.
Katika kikao maalum cha Baraza la Haki za Binadamu cha Umoja wa Mataifa kilichofanyika mjini Geneva, Ali Bahraini, balozi na mwakilishi wa kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, alieleza wasiwasi wake kuhusu njaa kali, wimbi la wakimbizi, na mateso ya raia wasio na hatia akisema hali hiyo ni miongoni mwa majanga mabaya zaidi ya kibinadamu duniani.
Bahraini alikosoa ukimya wa muda mrefu na kukosekana kwa hatua thabiti za kimataifa ambazo, kwa mujibu wake, zimechangia kuzorota kwa hali ya Sudan. Aliongeza kuwa uingiliaji wa madola ya kigeno, ikiwemo usambazaji wa silaha na kupelekwa kwa mamluki, unachochea mapigano na kuongeza mateso ya raia.
Akisisitiza ulazima wa kuheshimiwa kwa mamlaka na umoja wa ardhi ya Sudan, mwanadiplomasia huyo amesema Iran inapinga vikali jaribio lolote la kuanzisha “utawala mbadala” au kudhoofisha nguvu ya serikali halali ya Khartoum.
Iran imezitaka nchi zote kuchukua hatua madhubuti za kulinda raia na kuunga mkono amani na mshikamano wa kudumu nchini humo.
Katika kikao hicho cha 38 cha dharura cha Baraza la Haki za Binadamu, nchi washiriki pia zililaani uhalifu uliofanywa katika Al-Fasher na maeneo ya jirani, na kusisitiza haja ya kutafuta suluhu endelevu kwa mgogoro wa kibinadamu na kisiasa unaoendelea Sudan.
Mapigano nchini Sudan yalianza Aprili 2023 kati ya Jeshi la Serikali na waasi wa RSF wanaotaka kunyakua Madaraka. Serikali ya Sudan inaituhumu serikali ya Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) kuwa ndie muungaji mkono mkuu wa waasi wa RSF wanaotenda jinai nchini humo.