Umoja wa Mataifa: Israel imetenda jinai za kivita Ukanda wa Ghaza
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i130886-umoja_wa_mataifa_israel_imetenda_jinai_za_kivita_ukanda_wa_ghaza
Tume ya uchunguzi ya Umoja wa Mataifa imetangaza kwamba Israel imefanya mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina katika Gaza.
(last modified 2025-09-24T09:09:38+00:00 )
Sep 17, 2025 02:19 UTC
  • Umoja wa Mataifa: Israel imetenda jinai za kivita Ukanda wa Ghaza

Tume ya uchunguzi ya Umoja wa Mataifa imetangaza kwamba Israel imefanya mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina katika Gaza.

Mkuu wa Kamati ya Uchunguzi ya Umoja wa Mataifa ametangaza kuwa, utawala wa Israel umefanya jinai na mauaji ya halaiki katika Ukanda wa Gaza.

Navi Pillay ametangaza kuwa, utawala wa Kizayuni ulifanya mauaji ya halaiki katika Ukanda wa Gaza, na Benjamin Netanyahu akiwa Waziri Mkuu, Isaac Herzog akiwa rais wa utawala huo, na Yoav Gallant, Waziri wa zamani wa Ulinzi walihusika katika jinai hizo.

Kwa mujibu wa ripoti ya kamisheni hiyo, ushahidi uliopo unaonyesha kufanyika mauaji ya umati, kuzuia misaada, Wapalestina kuyahama makazi yao kwa lazima na uharibifu wa miundombinu ya afya unaofanywa na utawala wa Kizayuni. Aidha Pillay amesema, utawala wa Israel umefanya jinai nne kati ya tano za mauaji ya kimbari chini ya Mkataba wa 1948. Navi Pillay, mwenyekiti wa tume hiyo alilinganisha hali ya Gaza na mauaji ya halaiki ya Rwanda na kusema: "Wapalestina ndio walengwa wa mauaji haya ya kimbari."

Ripoti hii ndiyo msimamo mkali zaidi kuwahi kuchukuliwa na chombo cha Umoja wa Mataifa na inaweza kuathiri kesi inayoendelea ya mauaji ya kimbari dhidi ya utawala wa Kizayuni katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki.

Hayo yanajiri katika hali ambayo, Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF) umetangaza kuwa, hali ya watoto wa Kipalestina hususan katika Ukanda wa Gaza ni mbaya mno na kwamba, mtoto mmoja kati ya watano wa Kipalestina ana utapiamlo.

Ripoti ya UNICEF inaeleza kuwa, hali ya watoto katika Ukanda wa Gaza inazidi kuwa mbaya, na wanakabiliwa na hatari zaidi kutokana na vita, uvamizi wa Israel, na mzingiro mkali dhidi ya Ukanda wa Gaza.