Shambulio la Israel Doha laleta wasiwasi wa kugawika Misri vipande vipande
Baada ya utawala wa Kizayuni wa Israel kufanya shambulio la kigaidi huko Doha, mji mkuu wa Qatar, Waziri Mkuu wa Misri amesema kwamba nchi yake nayo inalengwa katika njama za kuchora upya ramani ya eneo la Asia Magharibi na kuna hatari ikagawika vipande vipande.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Fars, Waziri Mkuu wa Misri, Mostafa Kamal Madbouly amesema kwamba hofu hiyo iko katika ngazi ya ndani na kimataifa na ni katika changamoto za kikanda na kimataifa zinazoikabili Misri na eneo hili zima. Amesema hayo mbele ya viongozi waandamizi wa vyombo vya habari vya Misri.
Amesema anaamini kwamba hivi sasa dunia inapitia kipindi cha "kuzaliwa ramani mpya ya kijiografia na kisiasa na kwamba eneo la "Mashariki ya Kati" liko kwenye kitovu cha mabadiliko hayo.
Waziri Mkuu wa Misri amesisitiza kuwa, nchi yake sawa na nchi nyingine, inakabiliwa na changamoto tata zinazohitaji welewa wa umma na mshikamano wa ndani ili kulinda utulivu na usalama kitaifa.
Baada ya utawala wa Kizayuni kufanya shambulio la kigaidi la anga dhidi ya mji mkuu wa Qatar, Doha, kwenye eneo ilipokuwepo timu ya mazungumzo ya Hamas, Misri imetuma ujumbe rasmi kwa Marekani ikiionya isithubutu kufanya jinai kama hiyo kwenye ardhi ya Misri.
Cairo amesisitiza katika ujumbe huo kwamba "shambulio lolote la Israel dhidi ya viongozi wa harakati za Palestina katika ardhi ya Misri litakuwa na matokeo mabaya na ya maafa."
Vyanzo vya kidiplomasia vimeripoti kuwa, ujumbe huo ulifikishwa Washington kupitia njia rasmi na ulikuwa na msisitizo wa Misri wa kuhifadhi mamlaka yake ya kitaifa na usalama wa ndani kwa gharama yoyote ile.