Afrika Kusini yaitaka Israel iwaachie wanaharakati wa msafara wa Sumud
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i131522-afrika_kusini_yaitaka_israel_iwaachie_wanaharakati_wa_msafara_wa_sumud
Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa jana Alkhamisi alitaka kuachiliwa mara moja kwa Waafrika Kusini na raia wengine wa kigeni wanaozuiliwa na jeshi la Israel, baada ya wanajeshi wa majini wa utawala huo haramu kushambulia msafara wa kibinadamu uliokuwa unaelekea Gaza.
(last modified 2025-10-03T03:30:30+00:00 )
Oct 03, 2025 03:30 UTC
  • Afrika Kusini yaitaka Israel iwaachie wanaharakati wa msafara wa Sumud

Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa jana Alkhamisi alitaka kuachiliwa mara moja kwa Waafrika Kusini na raia wengine wa kigeni wanaozuiliwa na jeshi la Israel, baada ya wanajeshi wa majini wa utawala huo haramu kushambulia msafara wa kibinadamu uliokuwa unaelekea Gaza.

Ramaphosa amelaani shambulio hilo katika maji ya kimataifa, akisema linaonyesha kuendelea kwa Israel kupuuza sheria za kimataifa sanjari na kushtadi mgogoro wa kibinadamu katika eneo hilo la Palestina linalozingirwa.

"Kuzuiliwa kwa msafara wa kimataifa wa Sumud ni kosa jingine kubwa la Israel dhidi mshikamano wa kimataifa na hisia ambazo zinalenga kupunguza mateso huko Gaza, na kuendeleza amani katika eneo hilo," amesema Ramaphosa katika taarifa.

Rais huyo wa Afrika Kusini ameitaka Israel kuwaachilia huru mara moja raia waliokamatwa na askari wa Israel wakati wa uvamizi huo, na kuruhusu meli za misaada kupeleka mizigo yao kwa wakazi wa Gaza.

"Kwa niaba ya serikali na taifa letu, natoa wito kwa Israel kuwaachilia mara moja Waafrika Kusini waliotekwa nyara katika maji ya kimataifa, na kuwaachilia pia raia wengine ambao walikuwa wanajaribu kufika Gaza kupeleka msaada wa kibinadamu," amesema Ramaphosa.

Amesema kuwa, hatua za Israel zilikiuka uhuru wa nchi ambazo bendera zao zilipeperushwa kwenye meli za msafara wa Sumud na kukiuka amri ya Mahakama ya Kimataifa inayotaka kufikishwa misaada ya kibinadamu bila vikwazo huko Gaza.

"Afrika Kusini inaunga mkono wito wa Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Kibinadamu kwa Israel wa kuondoa haraka vikwazo vya Gaza, na kuruhusu kuingia kwa suhula na vifaa vya kuokoa maisha kwa njia zote zinazowezekana," ameongeza.

Amesema dhamira ya msafara wa Sumud ilikuwa njia moja ya kutangaza "mshikamano," na wala sio makabiliano, na ameonyesha matumaini kwamba Israel itawaachilia huru haraka wanaharakati iliowateka, akiwemo mjukuu wa Nelson Mandela, Mandla Mandela.