WFP: Kiwango cha chakula kinachoingizwa Gaza ni kidogo mno
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i132342-wfp_kiwango_cha_chakula_kinachoingizwa_gaza_ni_kidogo_mno
Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula (WFP) limetangaza kuwa, kiwango cha chakula kinachoingia Gaza bado kiko chini sana ya lengo la tani 2,000 kwa siku, likitoa wito kwa utawala wa Kizayuni wa Israel kufungua vituo zaidi vya mipakani.
(last modified 2025-10-24T05:41:31+00:00 )
Oct 24, 2025 04:19 UTC
  • WFP: Kiwango cha chakula kinachoingizwa Gaza ni kidogo mno

Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula (WFP) limetangaza kuwa, kiwango cha chakula kinachoingia Gaza bado kiko chini sana ya lengo la tani 2,000 kwa siku, likitoa wito kwa utawala wa Kizayuni wa Israel kufungua vituo zaidi vya mipakani.

WFP imesema kuwa ugavi wa chakula umeongezeka baada ya kusitishwa mapigano, lakini bado haujafikia kiwango kinachohitajika kwa sababu ni vituo viwili tu vya kuingia katika eneo la Palestina vinavyofanya kazi.

Kwa mujibu wa WFP, takriban tani 750 za chakula zinaingia Ukanda wa Gaza kila siku, lakini kiwango hicho bado ni kidogo mno ikilinganishwa na mahitaji makubwa baada ya vita vya miaka miwili vilivyoharibu sehemu kubwa ya Ukanda wa Gaza.

Abeer Etefa, msemaji wa WFP amesema, “Ili kufanikisha ongezeko hili, tunapaswa kutumia kila kituo cha mipaka kilichopo kwa sasa,” .

Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni, Benjamin Netanyahu, alisema Jumamosi kuwa mpaka wa Rafah kati ya Gaza na Misri utaendelea kufungwa hadi taarifa nyingine, na kufunguliwa kwake kutategemea Harakati ya Hamas kukabidhi miili ya mateka waliokufa.

Hayo yanajiri katika hali ambayo, ripota Maalumu wa Umoja wa Mataifa katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu ametoa ripoti yake mpya kuhusu mauaji ya kimbari ya utawala wa Kizayuni Israel katika Ukanda wa Gaza, na kutoa maelezo ya kina kuhusu ushiriki wa kimataifa katika ukatili wa Tel Aviv.

Karibu Wapalestina elfu 70 wameuawa katika kampeni ya mauaji ya kimbari ya Israel huko Gaza ikisaidiwa kwa hali na mali na madola ya Magharibi.