Umoja wa Mataifa: Hali ya kibinadamu Gaza ni mbaya
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i134202-umoja_wa_mataifa_hali_ya_kibinadamu_gaza_ni_mbaya
Umoja wa Mataifa umeonya kuhusu kuongezeka kwa janga la kibinadamu katika Ukanda wa Gaza kutokana na mvua na baridi kali huko Palestina.
(last modified 2025-12-12T02:40:33+00:00 )
Dec 12, 2025 02:40 UTC
  • Farhan Haq, Naibu Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa
    Farhan Haq, Naibu Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa

Umoja wa Mataifa umeonya kuhusu kuongezeka kwa janga la kibinadamu katika Ukanda wa Gaza kutokana na mvua na baridi kali huko Palestina.

Farhan Haq, Naibu Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, ametangaza kuwa, Gaza inakabiliwa na mfumo mpya wa hali ya hewa unaoongeza hatari ya hipothemia (kupungua kwa joto la mwili chini ya nyuzi joto 35 za Celsius) kwa watoto na watoto wachanga.

Afisa huyo wa Umoja wa Mataifa amesema, mamia ya familia zimehamishwa kutoka maeneo ya pwani yenye hatari ya mafuriko kwenda maeneo salama. Farhan Haq pia aliripoti kuendelea kwa usumbufu katika uingizaji wa vifaa vya kielimu Gaza, akiongeza kuwa tangu mwanzoni mwa Desemba, takriban watu 260,000 wamepokea msaada wa chakula kupitia vituo 60 vya usambazaji, ikiwemo kaskazini mwa Gaza.

Naibu Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, akiashiria ongezeko la matukio ya kiusalama ambayo, alisema, "yanatishia maisha ya raia na wafanyakazi wa misaada", alisema kwamba kituo cha afya huko Maghazi pia kililengwa katika saa za hivi karibuni katika eneo linalojulikana kama mpaka wa utenganishaji.

Wakati huo huo, msemaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Misaada na Ajira kwa Wakimbizi wa Palestina (UNRWA) amesema kwamba "kinachoendelea huko Gaza hakijawahi kushuhudiwa tangu wakati wa Vita vya Pili vya Dunia."

Katika upande mwingine, Wizara ya Afya ya Gaza imetoa taarifa inayoashiria ukosefu wa dawa na vifaa vya matibabu huko Gaza, na kusisitiza kuwa asilimia 52 ya orodha ya dawa muhimu, asilimia 71 ya orodha ya bidhaa za matibabu, na asilimia 70 ya vifaa vya maabara havipo kabisa huko Gaza.