Hamas yalaani mauaji ya kamanda wake, raia Gaza
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i134290-hamas_yalaani_mauaji_ya_kamanda_wake_raia_gaza
Kiongozi wa ngazi ya juu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas katika Ukanda wa Gaza, Khalil al-Hayya, katika taarifa yake ya video leo Jumapili amethibitisha kuwa, kamanda mwandamizi wa harakati hiyo, Raed Saed ni miongoni mwa watu watano waliouawa shahidi katika shambulio la Israel huko Gaza.
(last modified 2025-12-14T09:13:22+00:00 )
Dec 14, 2025 09:13 UTC
  • Hamas yalaani mauaji ya kamanda wake, raia Gaza

Kiongozi wa ngazi ya juu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas katika Ukanda wa Gaza, Khalil al-Hayya, katika taarifa yake ya video leo Jumapili amethibitisha kuwa, kamanda mwandamizi wa harakati hiyo, Raed Saed ni miongoni mwa watu watano waliouawa shahidi katika shambulio la Israel huko Gaza.

Hamas imethibitisha kuuawa kwa kamanda wake mkuu katika shambulio hilo la Wazayuni huko Gaza, hayo yakihesabiwa kuwa mauaji ya kiongozi wa hadhi ya juu zaidi wa Hamas tangu kufikiwa makubaliano ya kusitisha mapigano Gaza mwezi Oktoba.

"Kufuatia ukiukwaji unaoendelea wa Israel ikiwa ni pamoja na mauaji ya hivi karibuni ya kamanda wa Izzuddin Qassam, tawi la kijeshi la Hamas Raed Saed hapo jana, tunawaomba wapatanishi na haswa serikali ya Marekani na Rais wa nchi hiyo, Donald Trump kama mdhamini mkuu wa makubaliano hayo, kuilazimisha Israel iheshimu makubaliano ya kusitisha mapigano na kuyatekeleza," Khalil al-Hayya amesema katika taarifa ya video leo Jumapili.

Kwa akali, watu 25 walijeruhiwa katika shambulio hilo la hivi karibuni la utawala katili wa Israel huko Gaza.

Tangu kuanza kutekelezwa usitishaji mapigano mwezi Oktoba, Israel imeendelea kushambulia maeneo mbali mbali ya Gaza kila siku - zaidi ya mara 800, na kuua shahidi angalau watu 386 - katika ukiukaji wa wazi wa makubaliano, kwa mujibu wa mamlaka za Gaza.

Hamas imeilaani vikali Israel kwa kutotimiza wajibu wake katika makubaliano ya kusitisha mapigano huko Gaza, wakati harakati hiyo ya Palestina imetekeleza majukumu yake yote kwa mujibu wa awamu ya kwanza ya makubaliano hayo.

Abduljabbar Saeed, mwakilishi wa Ofisi ya Kisiasa ya Hamas amefafanua katika mahojiano na tovuti ya Quds News mijadala inayoendelea kuhusu awamu ya pili ya makubaliano ya kusitisha mapigano na suala la wapatanishi.

Amesema, pande zote zilizohusishwa katika makubaliano zimekubaliana kwamba utawala wa Israel haujatimiza majukumu mengi katika awamu ya kwanza ya usitishaji mapigano.