UN yaituhumu RSF kuwa imefanya "uhalifu wa kivita" huko El Fasher
-
Wapiganaji wa RSF
Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa amesema kwamba uhalifu unaofanywa na wapiganaji wa kundi la Rapid Support Forces (RSF) huko El Fasher nchini Sudan ni sawa na uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu.
Taarifa iliyotolewa jana Ijumaa na Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa UN ilisema kwamba mji huo ulitekwa na RSF Oktoba 2025, baada ya kuzingirwa kwa muda mrefu kulikoandamana na ukatili na mauaji ya raia.
Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa UN imeeleza kwamba nyaraka za uhalifu huo zimetegemea mahojiano yaliyofanywa na zaidi ya waathiriwa 140 na mashahidi katika Jimbo la Kaskazini mwa Sudan na mashariki mwa Chad, mwishoni mwa mwaka 2025, ikibainisha kuwa zaidi ya watu 6,000 waliuawa katika siku tatu za kwanza za shambulio la RSF huko El Fasher - mji mkuu wa Jimbo la Kaskazini mwa Darfur, magharibi mwa Sudan - baada ya kuzingirwa na waasi hao.
Ripoti hiyo imeongeza kuwa kwa uchache watu 4,400 waliuawa ndani ya mji, huku wengine zaidi ya 1,600 wakiuawa walipokuwa wakijaribu kukimbia. Ripoti hiyo imeonya kwamba idadi halisi ya watu waliouawa inaweza kuwa kubwa zaidi, ikizingatiwa kwamba maelfu hawajulikani walipo.
Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa amelituhumu kundi la waasi la Rapid Support Forces (RSF) - na washirika wake "wanamgambo wa Kiarabu" - kwa kufanya uhalifu mkubwa ikiwa ni pamoja na mauaji, mashambulizi ya makusudi na ya kiholela dhidi ya raia, utumiaji wa njaa kama silaha ya vita, pamoja na ukatili wa kingono, uporaji na kuajiri watoto kama wapiganaji vitani.