EU yakema vikali mashambulizi ya Saudia dhidi ya hospitali Yemen
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i13444-eu_yakema_vikali_mashambulizi_ya_saudia_dhidi_ya_hospitali_yemen
Msemaji wa Mkuu wa Siasa za Nje wa Umoja wa Ulaya amekemea vikali mashambulizi yaliyofanywa na Saudi Arabia dhidi ya hospitali nchini Yemen na kutoa wito wa kutatuliwa mgogoro wa nchi hiyo kwa njia za kisiasa.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Aug 17, 2016 09:32 UTC
  • EU yakema vikali mashambulizi ya Saudia dhidi ya hospitali Yemen

Msemaji wa Mkuu wa Siasa za Nje wa Umoja wa Ulaya amekemea vikali mashambulizi yaliyofanywa na Saudi Arabia dhidi ya hospitali nchini Yemen na kutoa wito wa kutatuliwa mgogoro wa nchi hiyo kwa njia za kisiasa.

Christos Stylianides ambaye pia ni Kamishna wa Misaada ya Kibinadamu na Usimamizi wa Migogo wa Umoja wa Ulaya amesema kuwa, mashambulizi ya anga dhidi ya shule na hospitali inayohudumia watu katika eneo la Abs huko kaskazini magharibi mwa Yemen ambayo yameua na kujeruhi watu wengi haviwezi kukubalika.

Stylianides ameongeza kuwa, mashambulizi hayo ni sehemu ya mlomlongo wa mashambulizi yanayolenga taasisi za huduma za afya, madaktari na shule nchini Yemen na kwamba kuna ulazima wa kufanyika uchunguzi kuhusu uhalifu huo.

stylianides

Taarifa iliyotolewa na afisa huyo wa ngazi za juu wa Umoja wa Ulaya imesisitiza kuwa: Mashambulizi yanayofanywa dhidi ya raia na vituo vya huduma za kijamii yanapingana na sheria za kimataifa.

Raia wasiopungua 25 wameuawa na wengine 20 wamejeruhiwa katika shambulio la anga la ndege za utawala vamizi wa Saudi Arabia dhidi ya hospitali Abs kaskazini mwa Yemen.