Mateka wa zamani wa Muisraeli huko Gaza: Ninapata amani ninaposikiliza Qur'ani
-
Emily Damari, mateka wa zamani wa Muisraeli huko Gaza:
Hadithi ya mateka wa zamani wa Hamas, Emily Damari imevuma tena katika vyombo vya habari katika tukio lililozua dhoruba ya hasira ndani ya duru za Israel na kwenda mbali zaidi hadi kutolewa wito mwanamke huyo arudishwe matekani huko Gaza!
Hadithi hiyo ilianza wakati rafiki yake Emily Damari aliporusha video kwenye Instagram inayomuonyesha akisikiliza Qur'ani Tukufu huku akiendesha gari. Awali, alithibitisha kwamba anapenda kusikiliza qiraa ya Qur'ani na kwamba anapata utulivu na amani ya nafsi kwa kusikiliza kitabu hicho kikisomwa licha ya ukweli kwamba, karibu mwaka na miezi sita umepita tangu aachiliwe huru kutoka Ukanda wa Gaza alikokuwa ametekwa na wapigania ukombozi wa Palestina wa harakati ya Hamas.
Mateka huyo wa zamani wa Israel anaonekana kwenye video akisikiliza kituo cha Redio Qur'ani Tukufu na kumwambia rafiki yake kwamba huwa anasikiliza kisomo cha Qur'ani anapokuwa peke yake ndani ya gari. Rafiki yake alimuomba azime redio, lakini alikataa na kumuomba yeye pia asikilize kisomo kitamu cha msomaji.
Wakati mazungumzo hayo yakiendelea ilikuwa ikisomwa Aya ya 104 ya Suratu Yunus inayosema: {Sema, "Enyi watu, ikiwa mnayo shaka kuhusu dini yangu, basi mimi siwaabudu wale mnaowaabudu badala ya Mwenyezi Mungu; lakini ninamwabudu Mwenyezi Mungu ambaye anawafisha, na nimeamrishwa niwe miongoni mwa mwenye kuamini."}
Mateka huyo wa zamani wa Hamas alitumia siku 471 (karibu mwaka 1 na miezi 4) akiwa chini ya ulinzi wa Brigedi za Qassam, tawi la kijeshi la Hamas huko Gaza, kabla ya kuachiliwa huru Januari 2025 kufuatia makubaliano ya kusitisha mapigano.
Baada ya kuachiliwa huru, Emily Damari alizungumzia jinsi watekaji wake walivyomtendea wema na kwamba walimpa matibabu mara kadhaa, ikiwa ni pamoja na baada ya kujeruhiwa kwa bomu la Israel lililolenga nyumba alikokuwa akishikiliwa. Mama yake aliviambia vyombo vya habari vya Israel kwamba alimkuta binti yake akiwa na afya njema zaidi kuliko alivyotarajia baada ya kuachiliwa huru.
Israel imekasirishwa sana na simulizi ya raia wake huyo na hata magazeti ya utawala huo yameutaja mkanda wa video hiyo kuwa propaganda inayounga mkono Hamas.