Sasa ni ruhsa kwa polisi wa Uturuki kuvaa Hijabu
Kwa mara ya kwanza, serikali ya Uturuki imetoa ruhusa kwa polisi wa kike kuvaa vazi la staha la Hijabu wakiwa kazini. Ruhusa hiyo imetolewa kupitia hukumu iliyotangazwa jana Jumamosi katika gazeti rasmi la serikali.
Kwa mujibu wa hukumu hiyo, wanawake wanaofanya kazi katika jeshi la polisi la Uturuki wanaweza kuvaa vilemba vya kustiri nywele zao chini ya kofia zao za kipolisi kwa sharti kwamba vilemba hivyo vifanane na rangi ya sare zao na visiwe na marembo yoyote. Hukumu zinazochapishwa kwenye gazeti rasmi la serikali nchini Uturuki huwa ni za kutekelezwa mara moja.
Ijapokuwa Uturuki ni nchi ya Kiislamu, lakini hadi hivi sasa vazi la Hijabu ni marufuku katika baadhi ya ofisi na taasisi za serikali. Mwaka 2010, Uturuki ilifuta marufuku ya kuvaa Hijabu iliyokuwa imewekwa kwenye vyuo vikuu vya nchi hiyo. Aidha uvaaji wa vazi la staha la Hijabu uliruhusiwa nchini Uturuki kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari katika miaka 2013 na 2014 kwa utaratibu.
Wapinzani wa Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki wanadai kuwa anafanya njama za kuvunja misingi yote ya usekulari iliyowekwa na Mustafa Kemal Atatürk wakati alipounda Jamhuri ya Uturuki mwaka 1923. Hata hivyo vyombo vya habari vinavyoiunga mkono serikali ya Uturuki vinasema kuwa, kuna nchi kadhaa za Magharibi nazo zimewapa idhini maafisa wao wa kijeshi kuvaa Hijabu, na Uturuki si ya kwanza kufanya hivyo.
Mwezi huu, polisi ya Scotland huko Uingereza ilitoa idhini kwa askari wa kike Waislamu kuvaa Hijabu wakiwa kazini. Serikali ya Canada nayo imetangaza kuwa, wiki hii itawaruhusu polisi wapanda farasi wa kikosi cha mfalme wa nchi hiyo kuvaa Hijabu wakiwa kazini kama njia ya kuongeza ubora wa utendaji kazi wao.