Mashambulio mapya ya Saudia yaua raia 12 nchini Yemen
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i14113-mashambulio_mapya_ya_saudia_yaua_raia_12_nchini_yemen
Watu wasiopungua 10 wameuawa katika mashambulio ya karibuni yaliyofanywa na ndege za kivita za Saudia katika eneo la Shar'ab mkoani Taiz nchini Yemen.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 28, 2016 03:06 UTC
  • Mashambulio mapya ya Saudia yaua raia 12 nchini Yemen

Watu wasiopungua 10 wameuawa katika mashambulio ya karibuni yaliyofanywa na ndege za kivita za Saudia katika eneo la Shar'ab mkoani Taiz nchini Yemen.

Kwa mujibu wa kanali ya televisheni ya Al-Masirah, watu wengine wasiopungua 11 wamejeruhiwa katika shambulio hilo.

Ndege za kivita za utawala vamizi wa Aal Saud zimeshambulia pia kwa mabomu ya vishada  kituo cha kijeshi cha al-Thu'ban  katika eneo la Usair kusini mwa Saudia ambacho kinadhibitiwa na wanamapambano wa Yemen.

Katika tukio jengine, shambulio la anga la ndege za kivita za Saudia limeua watu wawili na kujeruhi wengine wanane lilipolenga karakana ya mbao na gereji ya magari katika mji wa Abbas ulioko mkoani Hajjah.

Ndege za kivita za Saudia zimeshambulia pia mara 23 kituo cha jeshi la majini cha mji wa pwani wa Al-Hadidah huko magharibi mwa Yemen.

Ndege za kivita zinazoendelea kuua raia wasio na hatia Yemen

Wakati huohuo jeshi na vikosi vya kujitolea vya wananchi wa Yemen vimejibu hujuma za ndege za kivita za utawala vamizi wa Saudia kwa kuvishambulia kwa makombora ya Katyusha vituo viwili vya kijeshi vya al-Bahtit na al-Mantarah mkoani Jairan kusini mwa Saudia.

Wanamapambano wa Yemen wameshambulia pia matangi ya fueli ya shirika la mafuta la Saudia Aramco katika eneo la Jizan kusini mwa nchi hiyo.

Wanamapambano wa Ansarullah, Yemen

Tangu ulipoanzisha uvamizi wake wa kijeshi dhidi ya Yemen mnamo mwezi Machi mwaka uliopita, hadi sasa muungano vamizi wa kijeshi unaoongozwa na utawala wa Aal Saud na kuungwa mkono na Marekani umesha zishambulia skuli, hospitali, maeneo ya makaazi ya raia, barabara, masoko na kambi za wakimbizi na kuua maelfu ya raia wasio na hatia wa nchi hiyo.../