Israel yakasirishwa na ukosoaji wa UN kuhusu ujenzi haramu wa vitongoji
Utawala wa Kizayuni wa Israel umekasirishwa na ukosoaji wa hivi karibuni wa Umoja wa Mataifa kuhusu ujenzi haramu wa vitongoji unaofanywa na utawala huo ghasibu katika ardhi za Palestina unazozikalia kwa mabavu.
David Keyes, msemaji wa ofisi ya Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni amedai kupitia taarifa kuwa maelezo yaliyotolewa jana na Nickolay Mladenov, Mratibu Maalumu wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Mchakato wa Amani wa Mashariki ya Kati ni 'kichekesho' na kwamba yanaifanya amani iwe ngumu kupatikana kwa sababu yanapotosha historia na sheria za kimataifa.
Akihutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa hapo jana, Mladenov alisema upanuzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni umeongezeka kwa kasi katika kipindi cha miezi miwili iliyopita tangu ilipotolewa ripoti ya kuitaka Israel isimamishe shughuli hizo haramu za ujenzi katika ardhi za Palestina.
Ripoti hiyo ya kurasa nane ya jopo la pande nne za Umoja wa Mataifa, Marekani, Russia na Umoja wa Ulaya ilitolewa tarehe Mosi ya mwezi uliopita wa Julai. Ilielezwa katika ripoti hiyo kwamba upanuzi wa vitongoji unaofanywa na Israel, ubomoaji wa nyumba za Wapalestina na uporaji wa milki zao unavuruga uwezekano wa kile kinachoitwa suluhisho la uundaji madola mawili ya Israel na Palestina.
Tangu Julai Mosi utawala wa Kizayuni umeendeleza mipango yake ya kujenga nyumba 1,000 kinyume cha sheria huko Mashariki mwa Baitul Muqaddas na nyengine 735 katika Ufukwe wa Magharibi wa Mto Jordan.
Zaidi ya Wazayuni nusu milioni wanaishi kwenye vitongoji 230 vilivyojengwa kinyume cha sheria tangu Utawala wa Kizayuni wa Israel ulipoanza kuyakalia kwa mabavu maeneo ya Palestina ya Ufukwe wa Magharibi ikiwemo Baitul Muqaddas ya Mashariki kufuatia vita vya mwaka 1967.
Kwa mujibu wa sheria za kimataifa na maazimio ya Umoja wa Mataifa, ujenzi wa vitongozi unaofanywa na Israel katika ardhi za Palestina ni haramu, hata hivyo utawala huo ghasibu umeyadharau maazimio hayo na kuamua kuendeleza upanuzi wa vitongoji hivyo.../