Marekani yapendekeza kuiuzia Saudia silaha zenye thamani ya dola bilioni 115
Ripoti za siri zilizofichuliwa zinaeleza kuwa serikali ya Marekani imependekeza kuiuzia Saudi Arabia silaha zenye thamani ya dola bilioni 115.
Imeelezwa kuwa pendekezo hilo la uuzaji silaha ambalo ni la kiwango cha juu zaidi kupendekezwa na serikali ya Washington kwa utawala wa kifalme wa Aal Saud katika kipindi cha miaka 71 iliyopita linajumuisha silaha na zana za kivita pamoja na utoaji mafunzo ya kijeshi.
Ripoti hiyo iliyotayarishwa na Willliam Hartung, mtaalamu wa masuala ya silaha katika kituo cha sera za kimataifa inajumuisha mikataba 42 tofauti ambapo sehemu kuu ya mkataba huo bado haijawasilishwa kwa utawala wa Riyadh.
Hartung amevieleza vyombo vya habari kuwa ripoti hiyo inatazamiwa kutolewa leo.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari, tangu Barack Obama aingie madarakani Januari mwaka 2009, mapendekezo yaliyotolewa na Washington kuiuzia silaha Saudi Arabia yamejumuisha aina zote za zana za kijeshi zikiwemo silaha nyepesi, vifaru, helikopta za mashambulio, makombora ya angani kwa ardhini na makombora ya kujihami na mashambulio ya manowari. Washington imevipatia pia vikosi vya ulinzi vya Saudia mafunzo ya namna ya kuzitumia na kuzihifadhi silaha hizo.
Kwa mujibu wa William Hartung, kiwango cha silaha ambazo Marekani inaiuzia Saudia kinaweza kuwa wenzo mwafaka wa kuuwekea mashinikizo utawala wa Aal Saud.
Mwezi uliopita serikali ya Obama iliidhinisha msaada wa silaha kwa Saudi Arabia zenye thamani ya dola bilioni 1.1.
Silaha ambazo Washington imeiuzia Saudia zimekuwa zikitumiwa na utawala huo wa kifalme katika vita vyake vamizi dhidi ya Yemen.
Zaidi ya Wayemeni 10,000 wakiwemo wanawake na watoto wameshauawa hadi sasa tangu Saudia ilipoanzisha hujuma na mashambulio yake dhidi ya nchi hiyo mwezi Machi 2015.../