Sep 23, 2016 14:06 UTC
  • Amnesty yailaani Bahrain kwa kuidhinisha marufuku ya al-Wefaq

Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limelaani vikali hatua ya mahakama ya Bahrain kudhinisha marufuku ya chama kikuu cha upinzani nchini humo, al-Wefaq.

Katika Taarifa, mkuu wa utafiti katika Amnesty, Philip Luther amesema uamuzi wa kuidhinisha upigwaji marufuku al-Wefaq ni ukiukwaji wa wazi wa uhuru wa maoni na kukusanyika na ni jaribio la kukandamiza wakosoaji wa serikali ya Bahrain.

Luther amesema watawala wa nchi hiyo ndogo ya Ghuba ya Uajemi  wameshindwa kuwasilisha ushahidi wowote kuwa al- Wefaq si harakati ya  amani. Amesema al-Wefaq imekuwa ikijaribu kuleta mabadiliko Bahrain kutokana na kuongezeka ukandamizaji wa serikali.

Mwezi Juni mahakama moja ya Bahrain iliamuri kufungwa ofisi za al-Wefaq na kisha baada ya mwezi mmoja kupiga marufuku harakati hiyo ya upinzani kwa tuhuma kuwa inachochea ugaidi.

Sheikh Ali Salman

 

Hali kadhalika mwezi Juni mwaka  huu utawala wa Bahrain ulimpokonya uraia Sheikh Issa Qassim mwanazuoni mtajika wa Kishia, hatua ambayo ilikabiliwa na radiamali kali ya Mashia na ulimwengu mzima kwa ujumla.

Mwezi Mei Mahakama ya Rufaa ya Bahrain  ilizidisha hukumu ya kifungo cha jela cha miaka minne aliyokuwa amekatiwa Sheikh Ali Salman Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kiislamu ya Kitaifa ya al Wefaq hadi miaka tisa.

Bahrain imekuwa ikishuhudia maandamano ya amani ya wananchi dhidi ya utawala wa Aal Khalifa tangu mwezi Februari mwaka 2011. Wananchi wa Bahrain wanataka marekebisho ya kisiasa, huru, uadilifu, kukomeshwa vitendo vya ubaguzi na kuingia madarakani serikali iliyochaguliwa kwa njia ya kidemokrasia. Hata hivyo utawala wa Aal Khalifa siku zote umekuwa ukiwakandamiza raia, kuwaua na kuzuia maandamano yao ya amani.

 

Tags