Iraq yanasa magaidi waliopanga kutekeleza mashambulizi wakati wa Muharram
Wanachama wa kundi moja la kigaidi lililokuwa limepanga kufanya mashambulizi ya kigaidi katika mwezi wa Muharram wamekamatwa magharibi mwa mji mkuu wa Iraq, Baghdad.
Shirika la Upelelezi la Jeshi la Iraq limetangaza habari ya kutiwa mbaroni wanachama hao wa kundi moja la kigaidi katika eneo la al Ghazaliya magharibi mwa Baghdad na kueleza kuwa watu hao walikusudia kutekeleza mashambulizi dhidi ya raia na vyombo vya usalama katika mwezi wa Muharram huko Iraq.
Shirika la Upelelezi la Jeshi la Iraq limeongeza kuwa mbali na kuwakamata magaidi hao, wamenasa pia silaha nyingi, mabomu, zana mbalimbali, kompyuta na gari ambayo wamekuwa wakitumia katika oparesheni zao za kigaidi. Magaidi hao waliotiwa mbaroni wamekiri kuwa na uhusiano na kundi la Daesh na kwamba hadi sasa wameshafanya mashambulizi kadhaa ya kigaidi. Aidha wameeleza kuwa, lengo lao lilikuwa ni kutekeleza mashambulizi ya kigaidi katika maeneo mbalimbali ya raia huko Iraq katika mwezi wa Muharram.
Idadi kubwa ya waombolezaji wa Imam Hussein (a.s) kutoka Iran, Bahrain, Oman na nchi nyingine za Kiislamu tayari wameanza kuelekea katika mji wa Karbala huko Iraq kufuatia kuwadia mwezi wa Muharram.