Maelfu ya Wapalestina wasali Ijumaa katika msikiti mtukufu wa Al-Aqsa
Makumi ya maelfu ya Wapalestina wameshiriki kwenye Sala ya Ijumaa katika msikiti mtukufu wa Al-Aqsa licha ya vizuizi na hatua kali za usalama zilizochukuliwa na utawala wa Kizayuni katika mji wa Baitul Muqaddas, Palestina inayokaliwa kwa mabavu.
Khatibu wa Sala ya Ijumaa ya jana katika msikiti wa Al-Aqsa Sheikh Ikrimah Sabri aliwaeleza waumini walioshiriki kwenye ibada hiyo ya kimaanawi na kisiasa kuwa kuuhami na kuuunga mkono msikiti wa Al-Aqsa katika kukabiliana na hujuma za adui Mzayuni na walowezi haramu ni jukumu la Umma wa Kiislamu.
Sheikh Ikrima Sabri amesema baraza la mawaziri la utawala wa Kizayuni ndilo linalobeba dhima na mas-ulia ya mashambulio yanayofanywa na askari wa Israel na walowezi wa Kizayuni dhidi ya kibla hicho cha kwanza cha Waislamu.
Mkuu huyo wa Baraza Kuu la Kiislamu la Quds amesisitiza pia kuwa hata kama adui Mzayuni atashadidisha zaidi jinai zake, wananchi wa Palestina hawatofumbia macho hata chembe ndogo ya ardhi yao.
Mbali na Wapalestina wa Ufukwe wa Magharibi na Quds tukufu, waumini 236 kutoka Ukanda wa Gaza nao pia walifunga safari hadi mji huo wa Baitul Muqaddas unaokaliwa kwa mabavu kushiriki katika Sala ya Ijumaa ya juma hili.
Tangu ilipoanza Intifadha ya Quds mwezi Oktoba mwaka jana, mji wa Quds na msikiti wa Al-Aqsa zimekuwa uwanja wa mapigano makali na mlengwa wa mashambulio na hujuma kali za walowezi wa Kizayuni na askari wa utawala haramu wa Israel. Mapigano makali yamekuwa yakijiri pia baina ya askari wa Kizayuni na Waislamu wa Palestina wanaopigania haki yao ya kusali katika Masjidul Aqsa, kibla cha kwanza cha Waislamu.../