Bahrain yawahujumu Mashia wanaoomboleza
Kwa mara nyingine tena vyombo vya usalama vya utawala wa Aal-Khalifa nchini Bahrain vimewashambulia Waislamu wa madhehebu ya Shia wanaojumuika katika sehemu mbali mbali kwa ajili ya marasimu ya Ashura.
Maafisa wa polisi nchini humo wamehujumu vituo kadhaa walipokuwa wamekusanyika Waislamu hao katika kijiji cha al-Dair, kaskazini mashariki mwa nchi hiyo leo na kupelekea idadi ya hujuma za kinyama zilizotekelezwa na maafisa hao wa usalama wa Manama kufikia 35 katika muda wa wiki moja pekee.
Habari zinasema kuwa, polisi ya Bahrain imetumia mabomu ya kutoa machozi kuwatawanya Waislamu wa Kishia wanaokumbuka kuuawa shahidi Imam Hussein AS, mjukuu wa Mtume Mtukufu SAW.
Wakati huo huo, watawala wa Aal-Khalifa wametangaza marufuku ya kutosafiri kwa wanaharakati mashuhuri na watetezi wa haki za binadamu nchini humo, wakiwemo Mohammad Tajir, wakili wa haki za binadamu, Abdulnabi Al-Ekri na Sharaf Moussavi, maofisa kutoka shirika la kutetea haki za binadamu la Bahrain Transparency Society.
Hii ni katika hali ambayo, hivi karibuni wanazuoni wakuu wa Kiislamu nchini Bahrain walilaani ukandamizaji na dhulma zinazofanywa na watawala wa Aal-Khalifa dhidi ya Waislamu wa madhehenu ya Shia hususan wakati huu wanapofanya marasimu mbali mbali ya kukumbuka kuuawa shahidi Imam Hussein AS.
Taarifa ya maulamaa wa Bahrain imesema kuwa, hatua ya maafisa usalama wa Bahrain ya kuyavamia na kuyahujumu maeneo yanapofanyika marasimu hayo ya kidini ni kitendo kiovu, cha woga na kisichokubalika.