Palestina yaushtaki utawala wa Kizayuni kwa Umoja wa Mataifa
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i17098-palestina_yaushtaki_utawala_wa_kizayuni_kwa_umoja_wa_mataifa
Mamlaka ya Ndani ya Palestina imetuma ripoti kwa Umoja wa Mataifa ikiushitaki utawala wa Kizayuni wa Israel kwa kukanyaga sheria zote za kimataifa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 09, 2016 23:14 UTC
  • Palestina yaushtaki utawala wa Kizayuni kwa Umoja wa Mataifa

Mamlaka ya Ndani ya Palestina imetuma ripoti kwa Umoja wa Mataifa ikiushitaki utawala wa Kizayuni wa Israel kwa kukanyaga sheria zote za kimataifa.

Shirika la habari la Palestina MA'AN limeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, mwakilishi wa Palestina katika Umoja wa Mataifa Riyadh Mansour, ametuma barua tatu kwa Katibu Mkuu Ban Ki moon, na kwa mkuu wa Baraza la Usalama na pia kwa mkuu wa Baraza Kuu la umoja huo kulalamikia hali mbaya waliyo nayo Wapalestina katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Katika barua hizo, Riyadh Mansour amelalamikia hali mbaya ya Wapalestina wa mashariki mwa Quds, kuendelea vitendo vya ukandamizaji vya utawala wa Kizayuni dhidi ya taifa la Palestina, uvunjaji wa sheria na haki za binadamu, kuporwa ardhi za Wapalestina na mashambulizi ya kikatili yanayofanywa na Israel dhidi ya maeneo ya Wapalestina wakiwemo wale wanaoishi mashariki mwa Baytul Muqaddas.

Wazayuni wana faili jeusi la kufanya jinai za kila namna dhidi ya Wapalestina

 

Mwakilishi huyo wa Palestina katika Umoja wa Mataifa amesisitiza kuwa, utawala wa Kizayuni umekuwa ukikanyaga waziwazi sheria za kimataifa na kuitaka jamii ya kimataifa izidishe mashinikizo yake kwa Israel ili iache ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni kwenye maeneo wanayoporwa Wapalestina.

Aidha amesema, wakati umefika kwa jamii ya kimataifa kuchukua hatua za haraka kukabiliana na mipango ya kikoloni ya utawala wa Kizayuni katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu yakiwemo maeneo ya mashariki mwa mji wa Quds.