UN yalaani upanuzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i17434-un_yalaani_upanuzi_wa_vitongoji_vya_walowezi_wa_kizayuni
Kikao maalumu cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kimekosoa vikali kuendelezwa ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni na utawala ghasibu wa Israel katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 15, 2016 04:40 UTC
  • UN yalaani upanuzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni

Kikao maalumu cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kimekosoa vikali kuendelezwa ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni na utawala ghasibu wa Israel katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu.

Kikao hicho cha jana kisichokuwa rasmi kimefanyika katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York kufuatia ombi la nchi wanachama wa Baraza la Usalama zikiwemo Angola, Malaysia, Venezuela, Senegal na Misri. Aidha kikao hicho kilihudhuriwa na mashirika ya kimataifa ya kutetea haki za binadamu ikiwemo jumuiya ya Americans for Peace Now na shirika la B’Tselem, ambalo limekuwa likifuatilia jinai na uvunjwaji wa haki za binadamu unaofanywa na utawala haramu wa Israel huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu. Mashirika hayo yametoa wito wa kususiwa upanuzi wa vitongoji vya walowezi za Kizayuni katika ardhi za Wapalestina sambamba na kuyasusia mashirika yanayowekeza katika vitongoji hivyo.

Vitongoji haramu vya Israel katika ardhi ya Palestina

Hagai El-Ad, Mkurugenzi Mkuu wa shirika la B’Tselem amekiambia kikao hicho cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuwa, wakati umefika kwa umoja huo kuchukua hatua za makusudi huku akiikumbusha jamii ya kimataifa kuwa, "Wapalestina wanakabiliwa na hali ngumu na jinai za kutisha kila uchao na kuwa kila pumzi wanayovuta, wanavuta wakiwa ndani ya ardhi yao iliyoghusubiwa."

Zaidi ya Wazayuni nusu milioni wanaishi kwenye vitongoji 230 vilivyojengwa kinyume cha sheria tangu Utawala wa Kizayuni wa Israel ulipoanza kuyakalia kwa mabavu maeneo ya Palestina ya Ufukwe wa Magharibi ikiwemo Baitul Muqaddas ya Mashariki kufuatia vita vya mwaka 1967.