Mufti wa Syria awataka magaidi kujisalimisha huko Aleppo
Mufti wa Syria amewataka magaidi walioko nchini humo kujisalimisha wenyewe kabla ya kuanza operesheni kubwa na ya pande zote ya jeshi la nchi hiyo ya kukomboa kikamilifu maeneo yote ya mji huo.
Sheikh Ahmad Badreddin Hassoun amewataka magaidi wa kigeni walioko katika mji wa Aleppo waweke chini silaha zao na kujisalimisha wenyewe kwa serikali ya Syria au kurejea katika nchi zao.
Wapiganaji wa makundi ya kigaidi kama Daesh na Jabhatu Nusra wamekuwa wakipigana wao kwa wao katika maeneo ya mashariki mwa mji wa Aleppo baada ya kuhitilafiana juu ya suala la kuondoka katika mji huo.
Wapiganaji wa makundi hayo katika mji huo wa pili kwa ukubwa nchini Syria wanakabiliwa na mashambulizi makali ya jeshi la Syria na waungaji mkono wake.
Wakati huo huo gari moshi ya kwanza ilianza safari zake jana kati ya miji ya Homs na Tartus huko magharibi mwa Syria baada ya magaidi kufurushwa katika maeneo hayo. Safari za gari moshi kati ya miji hiyo miwili zilisimama tangu miaka mitano iliyopita kutokana na ukosefu wa usalama na mauaji ya kikatili yanayofanywa na magaidi wa makundi kama Daesh.