Ould Sheikh apinga serikali ya Uokovu wa Kitaifa Yemen
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i20449
Mjumbe wa Umoja wa Mataifa katika Masuala ya Yemen amedai kuwa hatua ya Harakati ya Ansarullah ya kuunda serikali mpya ya Uokovu wa Kitaifa nchini humo haiisaidii chochote nchi hiyo wala kusogeza mbele mchakato wa amani nchini humo.
(last modified 2025-07-19T08:58:23+00:00 )
Nov 30, 2016 04:09 UTC
  • Ould Sheikh apinga serikali ya Uokovu wa Kitaifa Yemen

Mjumbe wa Umoja wa Mataifa katika Masuala ya Yemen amedai kuwa hatua ya Harakati ya Ansarullah ya kuunda serikali mpya ya Uokovu wa Kitaifa nchini humo haiisaidii chochote nchi hiyo wala kusogeza mbele mchakato wa amani nchini humo.

Ismail Ould Sheikh Ahmad amedai kuwa hatua hiyo ya Harakati ya Ansarullah inatoa pigo kwa juhudi zilizofanyika hadi sasa kwa uungaji wa Umoja wa Mataifa kwa lengo la kuhitimisha mgogoro na vita vya miezi 20 huko Yemen. Mjumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Yemen pia amedai kuwa kundi la Ansarullah na chama cha Congresi ya Wananchi ya Yemen haviko kwa maslahi ya Wayemeni hivi sasa bali makundi hayo yanaifanya hali ya mambo nchini humo kuwa mbaya zaidi. Harakati ya Ansarullah na Congresi ya wananchi ya Yemen yenye mfungamano na Ali Abdallah Saleh juzi ziliasisi Serikali ya Uokovu wa Kitaifa ya nchi hiyo kwa kuhudhuriwa na mawaziri 42 chini ya uenyekiti wa Abdulaziz bin Habtoor  Mkuu wa serikali hiyo mpya.

Abdulaziz bin Habtoor Mkuu wa Serikali Mpya ya Uokovu wa Kitaifa ya Yemen

Mkuu wa Baraza Kuu la Mapinduzi Yemen amesema baraza la mawaziri litajumuisha majina yaliyowasilishwa na Harakati ya Ansarullah na  Chama cha Kongresi ya Wananchi na waitifaki wake.