Dec 04, 2016 07:58 UTC
  • Utawala wa Aal Khalifa waendelea kukiuka haki za binadamu

Utawala wa Aal Khalifa unaendelea kukiuka haki za binadamu kwa pande zote khususan katika upande wa kimadhehebu bila kujali lolote.

Bahrain inashuhudia mapambano ya wananchi dhidi ya utawala ulioko madarakani wa Aal Khalifa tangu mwezi Februari mwaka 2011 hadi sasa. Utawala wa Aal Khalifa  unaungwa mkono wazi wazi na Marekani, Uingereza na Saudi Arabia; na ushahidi wa wazi wa uungaji mkono huo pia ni kukaa kimya madola hayo ya Magharibi mkabala na  chokochoko za Aal Saud huko Bahrain, ukandamizaji wake kwa wananchi na wapinzani walio dhidi yake. 

Hatua hizo ambazo zaidi ya yote zinaungwa mkono na Waziri Mkuu wa Bahrain, zimekuwa sababu ya kukiukwa kwa pande zote haki za binadamu na utawala wa Aal Khalifa. Pamoja na hayo, utawala wa Aal Khalifa ambao unafuata siasa za Saudi Arabia na kufungamana na fikra za Kiwahabi, umesababisha mgawanyiko wa kimadhehebu huko Bahrain na hivyo kutoa zingatio mahasusi kwa ukiukaji wa haki za binadamu kwa upande wa kimadhehebu. Miongoni mwa ukiukaji huo wa haki za binadamu tunaweza kuashiria, kunyang'anywa uraia wanazuoni watajika wa Bahrain akiwemo Sheikh Issa Qassim na kuhukumiwa maulamaa mashuhuri wa nchi hiyo kama Sheikh Ali Salman Katibu Mkuu wa Jumuiya ya al Wifaq ya nchini humo. 

Utawala wa Aal Khalifa pia hautilii maanani malalamiko makubwa ya wananchi wa Bahran katika kuamiliana kwa mabavu na wanazuoni wa nchi hiyo. Wananchi wa Bahrain wameamua kuandamana kila siku mbele ya nyumba ya Shekh Issa Qassim baada ya mahakama moja inayofungamana na utawala wa Aal Khalifa mwezi Juni mwaka jana kuamuru kufutiwa uraia Sheikh Issa Qassim mwanazuoni mtajika wa nchini humo. Wananchi wa Bahrain wametaka kufutwa hukumu hiyo iliyotolewa kwa Sheikh Issa Qaasim na pia kusisitiza kufanyika  Swala ya Ijumaa chini ya uimamu wa mwanazuoni huyo mashuhuri. Hii ni katika hali ambayo, wanajeshi wa utawala wa Aal Khalifa juzi Ijumaa walizuia kufanyika Swala ya Ijumaa chini ya Uimamu wa Sheikh Qassim kwa wiki ya 25 mfululizo.

Sheikh Issa Qaasim mwanazuoni mashuhuri wa Bahrain 

Sheikh Ali Salman Katibu Mkuu wa Jumuiya ya al Wifaq ya Bahrain pia ni shakhsia mwingine ambaye amefungwa jela na utawala wa Aal Khalifa kwa mwaka wa pili sasa bila ya hata kujali maandamano makubwa yanayofanywa na wananchi wakimuunga mkono mwanazuoni huyo wa kidini. Sheikh Ali Salman alikamatwa na askari usalama wa Bahrain mwezi Disemba mwaka juzi. Mahakama moja ya Bahrain mwezi Julai mwaka jana ilimhukumu kifungo cha miaka minne jela Sheikh Ali Salman kwa tuhuma za kile ilichokitaja kuwa kuidharau Wizara ya Mambo ya Ndani na kuwachochea wananchi kuvunja sheria na kubadili utawala ulioko madarakani. Aidha katika hatua ya kushangaza, Mahakama ya Rufaa ya Bahrain iliongeza hukumu hiyo dhidi ya Sheikh Salman kwa kumhukumu kifungo kutoka miaka minne hadi miaka tisa. Wakati huo huo bila ya kuzingatia maandamano ya wananchi, utawala wa Bahrain  leo kwa mara nyingine tena unatazamiwa kuendesha kikao cha kesi ya kumhukumu Sheikh Issa Qassim huku mahakama ya rufaa pia ikitarajiwa kumhukumu mwanazuoni huyo. 

Sheikh Ali Salman Katibu Mkuu wa Jumuiya ya al Wifaq  ya Bahrain 

Tags