Tehran: Maajenti wa mauaji wanaituhumu Iran kukiuka haki
(last modified Tue, 18 Feb 2025 07:31:12 GMT )
Feb 18, 2025 07:31 UTC
  • Tehran: Maajenti wa mauaji wanaituhumu Iran kukiuka haki

Rais Masoud Pezeshkian wa Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu inatuhumiwa kukiuka haki za binadamu na pande ambazo zinasababisha vifo na uharibifu katika pembe mbali mbali za dunia.

Rais Pezeshkian amekosoa vikali unafiki wa maadui wa Jamhuri ya Kiislamu wanaoituhumu Iran kwa "kuunga mkono ugaidi" licha ya jitihada za Tehran za kukabiliana na jambo hilo ovu.

"Maadui wanadai kwamba wanatetea haki za binadamu na kuiita Iran kuwa 'taifa la kigaidi,' lakini ukweli ni kuwa, Iran ndio mhanga halisi wa ugaidi," Rais wa Iran alisema hayo katika hotuba yake hapa Tehran siku ya Jumatatu. 

Ameeleza bayana kuwa, "Kwa bahati mbaya, wale ambao wamevuruga amani ya eneo hili na ambao wanawapiga watu mabomu kwa urahisi na kuwazika chini ya vifusi; wale walioua zaidi ya watoto 18,000 wasio na hatia na wasio na ulinzi, na karibu wanawake 10,000 huko Gaza, wanadai kutetea haki za binadamu huku wakitutuhumu kuzikiuka."

Hotuba ya Pezeshkian imeangazia misimamo ya undumakuwili ya Marekani na waitifaki wake wa Magharibi na uungaji mkono wao kwa mashirika ya kigaidi kama vile kundi la kigaidi la Munafiqeen (MKO). Amesema kundi hilo linaloungwa mkono kwa hali na mali na Wamagharibi limerowa damu za maelfu ya raia na maafisa wa Iran mikononi mwake; na utawala wa Israel ambao umeua makumi ya maelfu ya watu katika eneo zima.

Akizungumzia ukatili unaoendelea kufanywa na utawala huo wa Kizayuni dhidi ya watu wasio na ulinzi wa Ukanda wa Gaza, Rais wa Iran amewalaani wale wanaojiita watetezi wa haki za binadamu kwa ukimya wao pamoja na kushiriki kwao katika jinai hizo.