Wazayuni wakivunjia tena heshima Kibla cha Kwanza cha Waislamu
Walowezi wa Kizayuni jana Jumapili waliingia kwenye eneo la Masjidul Aqswa, Kibla cha Kwanza cha Waislamu huko Palestina na kukivunjia heshima.
Kituo cha Habari cha Palestina kimeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, makuhani wa Kizayuni waliokuwa wanawaongoza walowezi hao wa Kizayuni walitoa maelezo ya kichochezi na ya kupotosha historia kuhusiana na hekalu la Nabii Sulaiman na ngano za Wazayuni, suala ambalo liliwakasirisha Waislamu na wanafunzi wa kidini wa Kiislamu waliokuwepo msikitini hapo.
Ikumbukwe kuwa utawala wa Kizayuni wa Israel unafanya njama za kila namna za kuubomoa kabisa Msikiti wa al Aqsa kwa madai kuwa eti umejengwa juu ya hekalu la Nabii Sulaiman, na mara kwa mara wamekuwa wakilivamia eneo la msikiti huo ili kufanikisha njama zao hizo.
Mwezi Oktoba 2016, walowezi elfu tatu wa Kizayuni waliuvamia Msikiti wa al Aqsa. Lengo kuu la njama hizo za Wazayuni ni kuwapokonya Waislamu eneo lao hilo takatifu na kufuta kabisa utambulisho wake wa Kiislamu na wa kihistoria. Shabaha nyingine ya Wazayuni hao ni kuligeuza eneo hilo kuwa nembo ya utawala wa Kizayuni.
Habari nyingine zinasema kuwa, jana Jumapili baadhi ya makaburi ya Waislamu maarufu kwa jina la Bab al Rahma yanayopakana na ukuta wa mashariki mwa Msikiti wa al Aqsa yalitekwa na wanajeshi katili wa utawala wa Kizayuni wa Israel.
Eneo la makaburi la Bab al Rahma ni katika maeneo ya kale zaidi ya Waislamu katika mji wa Baytul Muqaddas na ni sehemu ambayo wamezikwa masahaba wengi wa Bwana Mtume Muhammad SAW.