Umaskini waongezeka sana Ukanda wa Ghaza
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i23080-umaskini_waongezeka_sana_ukanda_wa_ghaza
Kituo cha Haki za Binadamu cha Palestina kimetangaza habari ya kuongezeka umaskini kwa asilimia 65 katika eneo la Ukanda wa Ghaza kutokana na kuendelea kuzingirwa kiuchumi kikamilifu eneo hilo na utawala wa Kizayuni.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 08, 2017 10:13 UTC
  • Umaskini waongezeka sana Ukanda wa Ghaza

Kituo cha Haki za Binadamu cha Palestina kimetangaza habari ya kuongezeka umaskini kwa asilimia 65 katika eneo la Ukanda wa Ghaza kutokana na kuendelea kuzingirwa kiuchumi kikamilifu eneo hilo na utawala wa Kizayuni.

Kituo hicho cha haki za binadamu huko Palestina kimeashiria katika ripoti yake mpya kuwa kiwango cha watu wasio na ajira huko Ghaza kimeongezeka kwa asilimia 47 na kwamba mahitaji ya kila siku ya asilimia 80 ya raia wa Kipalestina wakazi wa ukanda huo yanadhaminiwa na misaada kutoka nje. Ripoti hiyo imeongeza kuwa mzingiro wa kiuchumi wa miaka kumi wa Israel huko Ghaza unakiuka wazi haki za kiuchumi na kijamii za wakazi wa eneo hilo. 

Ripoti iliyotolewa na Kituo cha Haki za Binadamu cha Palestina imeendelea kubainisha kuwa,  ripoti ya Benki ya Dunia imeeleza kuwa, kiwango cha Wapalestina wasio na ajira katika mwezi Septemba mwaka jana kilikuwa asilimia 43 huku kiwango cha umaskini katika eneo hilo kikifikia zaidi ya asilimia 60.

Kivuko cha Rafah ambayo huwasaidia Wapalestina kuwasiliana na ulimwengu wa nje 

Utawala haramu wa Israel ulianza kulizingira eneo la Ukanda wa Ghaza tangu mwezi Januari mwaka 2006 kwa kuendesha mashambulizi ya anga, nchi kavu na baharini ili kuing'oa madarakani Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas; kufuatia ushindi ilioupata katika uchaguzi wa bunge.  Utawala wa Kizayuni pia unaendeleza mzingiro wake huo wa kidhulma dhidi ya raia wa Palestina wasio na hatia wa eneo hilo kwa kupuuza maazimio na sheria za kimataifa. Itafahamika kuwa, kivuko cha Rafah ni eneo pekee ambalo wakazi wa Ukanda wa Ghaza wanaweza kukitumia kufikia ulimwengu wa nje.