Jan 12, 2017 15:45 UTC
  • Jeshi la Lebanon: Ayatullah Rafsanjani alikuwa akihami Lebanon na Palestina

Kamanda Mkuu wa Jeshi la Lebanon amesema kuwa, marehemu Ayatullah Hashemi Rafsanjani, Mkuu wa Halmashauri ya Kuainisha Maslahi ya Mfumo wa Iran, alikuwa daima akichukua misimamo ya heshima katika kuihami Lebanon na Palestina katika kukabiliana na utawala haramu wa Kizayuni wa Israel.

Jean Kahwaji ameyasema hayo katika salamu za rambirambi alizozituma kwa Rais Hassan Rouhan wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambapo sambamba na kutoa mkono wa pole kufuatia kufariki dunia mwanazuoni huyo amesema kuwa faili la utumishi wa Sheikh Rafsanjani lilikuwa la mafanikio mengi katika kulitumikia taifa la Iran.

Sayyid Hassan Nasrullah, Katibu Mkuu wa Harakati ya Kiislamu ya Hizbullah.

Aidha kamanda wa Kahwaji ametaka kuendelezwa harakati endelevu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika maendeleo, ustawi na uthabiti. Kabla ya hapo Sayyid Hassan Nasrullah, Katibu Mkuu wa Harakati ya Kiislamu ya Hizbullah, Michel Aoun, Rais wa Lebanon, Saad Hariri, Waziri Mkuu na Nabih Berri, Spika wa Bunge la Lebanon kwa nyakati tofauti walitoa salamu za rambirambi kwa taifa la Iran kufuatia kufariki dunia Ayatullah Hashemi Rafsanjani, Mkuu wa Halmashauri ya Kuainisha Maslahi ya Mfumo wa Kiislamu.

Michel Aoun, Rais wa Lebanon

Ayatullah Hashemi Rafsanjani alifariki dunia Jumapili iliyopita akiwa na umri wa miaka 82, kwa maradhi ya moyo. Mbali na viongozi wa Lebanon, Jamhuri ya Kiislamu imeendelea kupata salamu za rambirambi kutoka viongozi wa pembe tofauti za dunia kufuatia msiba huo.

 Saad Hariri, Waziri Mkuu wa Lebanon

 

Tags