Askari wa Israel aliyeua Mpalestina afungwa miezi 18
Askari wa jeshi katili la utawala haramu wa Israel aliyemuua kwa kumfyatuliwa risasi raia wa Palestina, amehukumiwa kifungo cha miezi 18 pekee jela.
Jaji Maya Heller wa Mahakama ya Kijeshi ya Israel ametoa hukumu hiyo leo Jumanne, licha ya waendesha mashtaka kutaka mwanajeshi huyo ahukumiwe kifungo cha miaka mitatu hadi mitano jela.
Hata hivyo mawakili wa askari huyo Sajenti Elor Azaria, waliitaka mahakama hiyo ya kijeshi imuachie huru mteja wao wakidai kuwa alitekeleza mauaji hayo ili kunusuru maisha yake. Hii ni katika hali ambayo, mashuhuda wanasema kuwa kijana huyo wa Kipalestina Abdul Fattah al-Sharif, hakuwa amejizatiti kwa silaha yoyote alipouawa kwa kumiminiwa risasi na askari huyo wa Israel, mwezi Machi mwaka jana.

Awali, Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel alikuwa ametoa wito wa kuachiwa huru askari huyo, akidai kuwa alilazimika kutumia bunduki yake ili kujilinda na kuyanusuru maisha yake baada ya Mpalestina huyo kutaka kumshambuliwa kwa kisu.
Hata hivyo, rekodi ya kamera za siri za CCTV imeonyesha kuwa Mpalestina huyo alikuwa amelala chini kifudifudi wakati mwanajeshi huyo katili wa Israel alipomuua kwa kummiminia risasi.
Sari Bashi, Mkurugenzi wa shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch katika eneo la Mashariki ya Kati amekosoa vikali hukumu hiyo, aliyoitaja kuwa ni sawa na 'mamlaka za Israel kutuchezea shere'. Amesema hukumu hiyo itafungua mlango wa kuuawa Wapalestina zaidi kiholela katika siku zijazo.