Waziri wa Palestina: Israel inataka kuubomoa msikiti wa al-Aqswa
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i25702-waziri_wa_palestina_israel_inataka_kuubomoa_msikiti_wa_al_aqswa
Waziri wa Waqfu na Masuala ya Kidini wa Palestina ametahadharisha kuhusiana na njama za utawala wa Kizayuni wa Israel za kutaka kuubomoa msikiti mtakatifu wa al-Aqswa kibla cha kwanza cha Waislamu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 27, 2017 04:22 UTC
  • Waziri wa Palestina: Israel inataka kuubomoa msikiti wa al-Aqswa

Waziri wa Waqfu na Masuala ya Kidini wa Palestina ametahadharisha kuhusiana na njama za utawala wa Kizayuni wa Israel za kutaka kuubomoa msikiti mtakatifu wa al-Aqswa kibla cha kwanza cha Waislamu.

Sheikh Yousif Ideis amesema kuwa, utawala haramu wa Israel umekuwa ukifanya njama za kuubomoa msikiti huo mtakatifu kutokana na kuchimba kwake kila siku mashimo kuuzunguka msikiti huo.

Waziri huyo wa Palestina ameonya kuwa, hatua hizo za utawala vamizi wa Israel za kuchumba mashimo na njia za chini kwa chini katika maeneo ya kando kando na msikiti huo zitalitumbukiza eneo la Mashariki ya Kati katika vita na mapigano na Israel ndio ambayo itakuwa imewashwa moto wa vita hivyo.

Wanajeshi wa Israel wakiuvamia msikiti wa al-Aqswa

Sheikh Yousif Ideis amesisitiza kwamba, hatua hizo za utawala wa Kizayuni wa Israel zinakinzana wazi wazi na maazimio ya kimataifa kama azimio la hivi karibuni la Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) ambalo lilithibitisha tena kwamba msikiti mtukufu wa Al-Aqsa, kibla cha kwanza cha Waislamu ni milki ya Waislamu.

Baada ya kupasishwa kwa azimio hilo, Baitul Muqaddas Mashariki ikasajiliwa rasmi kuwa turathi ya Ulimwengu wa Kiislamu.

Weledi wa mambo katika Ulimwengu wa Kiislamu wanasema kuwa, Israel imekuwa ikifuatilia malengo kadhaa katika hatua zake hizo za kuchimba mashimo na njia za chini kwa chini kuelekea katika msikiti wa al-Aqswa ambapo moja ya malengo makuu ni kubomoa moja ya majengo muhimu ya Kiislamu huko Palestina.