Assad: Wanajeshi wa Marekani, Uturuki wamevamia Syria
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i26254-assad_wanajeshi_wa_marekani_uturuki_wamevamia_syria
Rais Bashar Assad wa Syria amesema wanajeshi wote wa kigeni waliongia nchini humo bila idhini ya seirikali ya Damascus ni wavamizi.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Mar 12, 2017 03:00 UTC
  • Assad: Wanajeshi wa Marekani, Uturuki wamevamia Syria

Rais Bashar Assad wa Syria amesema wanajeshi wote wa kigeni waliongia nchini humo bila idhini ya seirikali ya Damascus ni wavamizi.

Katika mahojiano na Televisheni ya PHOENIX ya China, Assad amesema serikali yake kamwe haijatoa idhini kwa wanajeshi wa Marekani ambao hivi karibuni wameingia katika mji wa Manbij kaskazini mwa Syria.

Amesisitiza kuwa, wanajeshi wowote wa kigeni wanaoingia Syria bila kualikwa, mashauriano au idhini ni wavamizi sawa wake ni Wamarekani, Waturuki au wengineo.

Amesema wanajeshi wa Marekani walioingia Syria kwa kisingizio cha kupambana na magaisi wa ISIS hawawezi kusaidia chochote kwani Wamarekani wamepoteza karibu kila vita walivyoingia kupigana.

Wanajeshi wa Marekani

Amesema historia inaonyesha kuwa, kila sehemu Marekani inapotumia wanajeshi wake hali huwa mbaya zaidi.

Siku chache zilizopita, Wizara ya Ulinzi ya Marekani ilitangaza kuwa imetuma wanajeshi wake nje na ndani ya mji wa Manbij ili kuzuia mapigano baina ya wanajeshi wa Uturuki na wanamgambo wanaopata himaya ya Marekani katika eneo hilo.

Kwingineko katika mahojiano yake, Assad amesisitiza kuwa mgogoro wa Syria utatatuliwa tu kwa njia ya mazungumzo sambamba na vita dhidi ya ugaidi. Aidha amesema kutafanyika kura ya maoni ili watu wa Syria waamue mfumo wanoautaka. Assad amesema vikosi vya jeshi la serikali vinakaribia kuukomboa mji wa Raqqa ambao magaidi wa ISIS waliutangaza kuwa mji mkuu wa utawala wao.