Wapinzani wa Syria wakataa mapendekezo ya mjumbe wa UN
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i26968-wapinzani_wa_syria_wakataa_mapendekezo_ya_mjumbe_wa_un
Duru za kuaminika zimeripoti kuwa ujumbe wa wapinzani wa serikali ya Syria katika mazungumzo ya amani ya nchi hiyo umeikataa hati ya mapendekezo iliyowasilishwa na mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya nchi hiyo Staffan De Mistura.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 28, 2017 11:51 UTC
  • Wapinzani wa Syria wakataa mapendekezo ya mjumbe wa UN

Duru za kuaminika zimeripoti kuwa ujumbe wa wapinzani wa serikali ya Syria katika mazungumzo ya amani ya nchi hiyo umeikataa hati ya mapendekezo iliyowasilishwa na mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya nchi hiyo Staffan De Mistura.

Duru za kuaminika za wapinzani wa Syria zimetangaza kuwa De Mistura amewasilisha kwa wapinzani wa serikali ya Damascus hati kuhusu maudhui nne zinazohusiana na nchi hiyo lakini ujumbe wa wapinzani umekataa kuidhinisha hati hiyo.

Kwa mujibu wa duru hizo, hati hiyo inajumuisha maudhui nne muhimu za serikali ya mpito, katiba, uchaguzi na suala la kupambana na ugaidi. Mjumbe maalumu wa UN amezitaka pande mbili zinazopigana nchini Syria  za serikali na wapinzani kutoa maoni na mapendekezo yao kuhusiana na hati hiyo.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Russia la Sputnik, miongoni mwa masuala muhimu zaidi yaliyozungumziwa kwenye hati iliyopendekezwa na Staffan De Mistura ni serikali ya mpito na taasisi zinazohusiana na serikali hiyo pamoja na utaratibu wake wa utendaji.

Staffan De Mistura

Hati hiyo aidha mbali na kutoa mapendekezo kuhusu katiba na kufanyika uchaguzi chini ya usimamizi wa Umoja wa Mataifa imependekeza pia masuali yanayohitaji maoni na majibu kuhusu madaraka na mamlaka ya serikali katika kupambana na ugaidi na msaada wa kimataifa katika suala hilo, suala la haki za binadamu, masuala yanayohusiana na usalama na uwepo wa vikosi vya kigeni nchini Syria .

Duru ya tano ya mazungumzo ya kusaka amani ya Syria ilianza Alkhamisi iliyopita mjini Geneva, Uswisi kwa mazungumzo ya utangulizi baina ya Naibu wa De Mistura Ramzi Ezzuddin Ramzi na jumbe za pande zote zilizohudhuria duru hiyo ya mazungumzo.../