UNHCR: Idadi ya wakimbizi wa Syria imevunja rekodi, yapindukia milioni 5
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i27054-unhcr_idadi_ya_wakimbizi_wa_syria_imevunja_rekodi_yapindukia_milioni_5
Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) limesema idadi ya raia wa Syria walioikimbia nchi na kwenda kutafuta hifadhi katika nchi nyingine imepindukia watu milioni 5.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Mar 30, 2017 10:49 UTC
  • UNHCR: Idadi ya wakimbizi wa Syria imevunja rekodi, yapindukia milioni 5

Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) limesema idadi ya raia wa Syria walioikimbia nchi na kwenda kutafuta hifadhi katika nchi nyingine imepindukia watu milioni 5.

Babar Baloch, Msemaji wa UNHCR amesema mbali na Syria kuwa na wakimbizi zaidi ya milioni 5 nje ya nchi, ina wakimbizi wa ndani wapatao milioni 6.3 ambao wamekimbia makazi yao wakihofia usalama wao, tangu mgogoro huo uanze miaka sita iliyopita.

Amesema kuwa, mwaka mmoja uliopita, idadi ya wakimbizi raia wa Syria waliokua nje ya nchi ilikuwa watu milioni 4.8 lakini kwa sasa idadi hiyo imepindukia watu milioni 5.

Wakimbizi wa Syria wanaoishi kambini

Mgogoro wa Syria ulianza mwaka 2011 kufuatia mashambulizi makubwa ya makundi ya kigaidi yakiungwa mkono na Saudi Arabia, Marekani na waitifaki wao kwa lengo la kuing'oa madarakani serikali halali ya nchi hiyo inayoongozwa na Rais Bashar al Assad, hujuma ambazo hadi sasa zimeshindwa kufikia malengo yake haramu.

Hivi karibuni, Sergey Shoygu, Waziri wa Ulinzi wa Russia alisema kuwa, muungano eti unaopambana na kundi la kigaidi la Daesh unaoongozwa na Marekani haujawa na nafasi yoyote chanya katika kupambana na ugaidi nchini Syria, bali hatua hiyo imezidi kuuvuruga mgogoro wa nchi hiyo ya Kiarabu.