Adiis: Jinai za Israel dhidi ya Msikiti wa al Aqsa zimeongezeka
Waziri wa Waqfu na Masuala ya Kidini wa Palestina amesema jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel limefanya uhalifu 99 wa aina mbalimbali dhidi ya Msikiti wa al Aqsa na Haram ya Nabii Ibrahim katika mwezi uliopita wa Machi pekee.
Taarifa iliyotolewa na Yusuf bin Adiis imeashiria mashambulizi yanayofanywa mara kwa mara na Wazayuni wa Israel dhidi ya maeneo matakatifu ya Palestina kwa kisingizio cha kutekeleza taratibu za kidini na kusema: Taasisi za Kizayuni za Israel zimezidisha mashambulizi dhidi ya Msikiti wa al Aqsa katika sikukuu ya Pasaka.
Waziri wa Waqfu wa Palestina ameongeza kuwa, utawala wa Kizayuni wa Israel umewatia nguvuni walinzi wa Msikiti wa al Aqsa na Haram ya Nabii Ibrahim katika mji wa al Khalil kwa shabaha ya kuvunja upinzani na mapambano ya Waislamu wa Palestina dhidi ya hujuma za Wazayuni.
Amesema kuwa mashambulizi na uhalifu wa Wazayuni dhidi ya maeneo matakatifu ya Quds vinahatarisha mustakbali wa eneo hilo tukufu. Ameongeza kuwa, Israel inatumia kimya cha nchi za Kiarabu na jamii ya kimataifa kwa ajili ya kuendelea mipango na njama zake za kuikalia kikamilifu Quds na Msikiti mtakatifu wa al al Aqsa ambacho ni kibla cha kwanza cha Waislamu.