Waislamu duniani washerehekea siku ya kupewa Utume Nabii Muhammad (saw)
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i28240-waislamu_duniani_washerehekea_siku_ya_kupewa_utume_nabii_muhammad_(saw)
Waislamu wa maeneo mbalimbali ya dunia wameungana katika kusherehekea siku ya kubaathiwa Mtume Muhammad (saw).
(last modified 2026-03-03T12:46:59+00:00 )
Apr 25, 2017 10:37 UTC
  • Waislamu duniani washerehekea siku ya kupewa Utume Nabii Muhammad (saw)

Waislamu wa maeneo mbalimbali ya dunia wameungana katika kusherehekea siku ya kubaathiwa Mtume Muhammad (saw).

Waislamu katika mji mkuu wa Azerbaijan, Baku wameungana na Waislamu mbalimbali duniani katika sherehe hizo ambapo sambamba na kusoma mashairi ya kumsifu Mtume huyo mwokozi wa walimwengu, wametoa ujumbe kwa ulimwengu wa Kiislamu kudumisha amani na upendo.

Katika marasimu hayo, Ayatullah, Ujagh Nejad, mwakilishi wa Faqihi Mtawala nchini Azerbaijan, mbali na kutoa mkono wa salamu za kheri na fanaka kwa mnasaba wa siku hii adhimu, ametoa historia ya shakhsia ya Mtume Muhammad (saw) kama nembo ya ruwaza njema kwa mwanadamu na kuwausia Waislamu wote kumfuata Nabii huyo wa Allah. Kadhalika mamia ya Waislamu wa Palestina wamemiminika katika msikiti wa al-Aqsa kwa ajili ya kuadhimisha sherehe hiyo. Shaykh Yusuf Abu Sneina, Imamu wa Msikiti wa al-Aqsa sambamba na kusisitizia juu ya utambulisho wa Uislamu na msikiti huo, amesema kuwa, bila shaka yoyote eneo hilo linahusiana na Waislamu. Mbali na Azerbaijan na Palestina, mataifa mbalimbali ya Kiislamu na Kiarabu kama vile Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Iraq, Yemen, Lebanon, Indonesia, Malaysia na kadhalika yameadhimisha sherehe hiyo ambayo inatambuliwa kama Iddi.

Msikiti wa Mtume Muhammad (saw)

Hii ni katika hali ambayo usiku wa kuamkia leo, Waislamu wa Suni nao waliadhimisha usiku wa Israa na Miraj, ambapo inakumbushia tukio la kusafirishwa na Malaika Jibril Nabii huyo wa Allah kutoka msikiti mtukufu wa Makka hadi msikiti wa Baytul-Maqdis na kutoka hapo hadi mbingu ya saba. Mtume Muhammad (s.a.w) alibaathiwa akiwa na umri wa miaka 40.