Yemen katika muelekeo wa mfumo wa kisiasa unaofanana na wa Libya
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i29028-yemen_katika_muelekeo_wa_mfumo_wa_kisiasa_unaofanana_na_wa_libya
Ushahidi uliopo unaonyesha kuwa Yemen inaelekezwa kwenye muundo na mfumo wa kisiasa sawa na uliofeli na kugonga mwamba nchini Libya.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 13, 2017 07:13 UTC
  • Yemen katika muelekeo wa mfumo wa kisiasa unaofanana na wa Libya

Ushahidi uliopo unaonyesha kuwa Yemen inaelekezwa kwenye muundo na mfumo wa kisiasa sawa na uliofeli na kugonga mwamba nchini Libya.

Hivi karibuni, Aidaroos Al-Zubaidi, mkuu wa mkoa aliyeuzuliwa katika eneo la Aden kusini mwa Yemen, alitangaza kuwa ameunda baraza la kisiasa lenye wajumbe 26 wakiwemo wakuu watano wa mikoa ya eneo hilo la kusini na mawaziri wawili wa serikali iliyojiuzulu ya aliyekuwa rais wa nchi hiyo AbdRabbuh Mansour Hadi.

Tangu mwezi Agosti mwaka uliopita wa 2016 hadi sasa mlango wa mazungumzo ya aina yoyote kati ya makundi ya Yemen umefungwa. Badala yake, yamejitokeza mazingira ya kuufanya mgogoro wa nchi hiyo uwe tata zaidi. Utata huo wa mgogoro wa kisiasa nchini Yemen unauelekeza muundo na mfumo wa kisiasa wa nchi kwenye hali sawa na iliyoshuhudiwa katika miaka mitatu ya karibuni nchini Libya, ambayo bila ya shaka kinyume na Libya inaweza kuwa na matokeo tofauti nchini Yemen.

Aidaroos al-Zubaidi (kulia)

Mnamo mwaka mmoja uliopita, Yemen imekuwa kwa namna fulani ikiendeshwa na serikali mbili tofauti. Kwa upande mmoja, serikali iliyojiuzulu ya Mansour Hadi, ambayo inatambuliwa rasmi na waungaji mkono wake wa Kiarabu na wa Magharibi ingali inaendelea na shughuli zake; tab'an inafanyia baadhi ya vikao vyake Riyadh, mji mkuu wa Saudi Arabia ili kuthibitisha kuwa ni serikali kibaraka na tegemezi kwa utawala wa Aal Saud. Na kwa upande mwengine, harakati ya Ansarullah na Kongresi ya wananchi inayoongozwa na Ali Abdullah Saleh, ambayo tangu AbdulRabbuh Mansour Hadi alipojiuzulu kimaonyesho  Januari 2015 ndizo zilizoshika hatamu za madaraka kaskazini mwa Yemen, mwezi Agosti mwaka jana ziliunda Baraza Kuu la Kisiasa katika mji mkuu Sana'a, na hatimaye mwezi Novemba zikaunda serikali ya uokovu wa kitaifa. Japokuwa kinyume na serikali iliyojiuzulu ya Mansour Hadi nchi za Kiarabu na za Magharibi haziitambui rasmi serikali ya uokovu wa kitaifa, lakini serikali hiyo ndiyo inayoungwa mkono na wananchi waliowengi ya Yemen. Kwa hivyo inapasa tuseme kuwa tangu mwezi Novemba mwaka 2016 hadi sasa, Yemen imekuwa ikiongozwa na serikali mbili huku ikishuhudia mamlaka mbili kinzani za utawala.

Wanamapambano wa harakati ya Ansarullah

Hivi sasa kuundwa  baraza la kisiasa la wajumbe 26 chini ya uongozi wa Idarus Al-Zubeidi na ambalo linaungwa mkono na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), kunadhihirisha kuwa kivitendo Yemen inaendeshwa na serikali tatu kwa wakati mmoja; hali inayoendelea pia kushuhudiwa nchini Libya. Libya nako kumeundwa serikali mbili, moja ikiwa na makao yake katika mji wa Tobruk na nyengine katika mji mkuu Tripoli, mbali na serikali ya uokovu wa kitaifa inayoungwa mkono na jamii ya kimataifa.

Hata hivyo kuna kitu kimoja kinachoitofautisha Yemen na Libya, ambayo ni uwezekano mkubwa wa Yemen kugawanyika na kuwa nchi mbili, kwa sababu kinyume na Libya, kabla ya muongo wa 1990 ardhi ya Yemen ilikuwa na mataifa mawili ya Yemen ya Kusini na Yemen ya Kaskazini ambazo ziliungana Aprili 22 mwaka 1990 na kuunda Jamhuri ya Yemen.

Hivi sasa zinaonekana ishara za Yemen ya Kusini kujitenga na Kaskazini; na kuundwa baraza la kisiasa la wajumbe 26  kunaweza kulipa nguvu zaidi suala hilo. Kwa sababu hiyo Muhammad Abdussalam, msemaji rasmi wa harakati ya Ansarullah ya Yemen ameonya kuhusiana na kuundwa baraza la kisiasa kwa ajili ya uendeshaji wa masuala ya eneo la kusini mwa nchi hiyo na kusisitiza kuwa hatua hiyo inatishia umoja  wa ardhi yote ya Yemen. Kabla ya hapo, kundi moja la viongozi wa maeneo ya kusini, ambao hivi sasa wako mji mkuu Sana'a, nao pia walisisitiza kuwa kuundwa baraza la kisiasa la kuendesha masuala ya kusini mwa Yemen ni njama za Umoja wa Falme za Kiarabu, Imarati za kulitenganisha eneo la kusini na ardhi yote ya Yemen ili kuzidhibiti ardhi za eneo hilo.

Msemaji wa Ansarullah, Muhammad Abdussalam

Nukta nyengine ni kuwa kuwepo serikali tatu nchini Libya kumekuwa sababu kuu ya kushindwa kuundwa serikali ya kitaifa nchini humo. Kwa hivyo harakati inayoshuhudiwa hivi sasa nchini Yemen ya kuielekeza nchi hiyo kwenye muundo na mfumo kama wa Libya kunaweza kukwamisha kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa huko Yemen na kuzidi kurefuka mgogoro wa kisiasa na kiusalama wa nchi hiyo.../