Magaidi zaidi ya 140 wa Daesh waangamizwa Mosul, Iraq
Kamanda wa Polisi Kuu ya Iraq ametangaza kuwa zaidi ya magaid 140 wa kundi la ukufurishaji la Daesh (ISIS) wameangamizwa katika eneo la Al-Haramat magharibi mwa mji wa Mosul.
Televisheni ya Sky News imemnukuu Shakir Jawaddat, kamanda wa polisi kuu ya Iraq akiripoti kuwa idadi kubwa ya magaidi wa kundi la kitakfiri la Daesh wameuawa katika operesheni ya shambulio lililofanywa na vikosi vya polisi ya taifa magharibi mwa mji wa Mosul, ambapo baadhi ya magaidi hao walikuwa wamejifunga mikanda ya mada za miripuko.
Kwa mujibu wa Shakir Jawaddat, magaidi hao wa kundi la ukufurishaji la Daesh walikuwa wamekusudia kujiripua kwa mada hizo za miripuko ili kuvizuia vikosi vya Iraq visiweze kusonga mbele.
Jawaddat ameongeza kuwa katika operesheni ya vikosi vya Iraq katika eneo la Al-Haramat magari zaidi ya 40 yaliyokuwa yametegwa mabomu yaliteketezwa na mamia ya mabomu yaliyotegwa ardhini yaliteguliwa.
Wakati huohuo Wahhab al-T'ai, mshauri wa masuala ya habari wa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Iraq amesema, zaidi ya asilimia 90 ya mji wa Mosul imekombolewa kutoka kwenye makucha ya kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh.
Operesheni ya kuukomboa mji wa Mosul, makao makuu ya mkoa wa Nainawa ilianza mwezi Oktoba mwaka uliopita wa 2016. Eneo la mashariki ya Mosul tayari imeshakombolewa na operesheni ya kulikomboa eneo la magharibi mwa mji huo ingali inaendelea.../